MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dkt. Joachim Eyembe amesema tangu, kuanza kutolewa kwa huduma ya Mama na Mtoto Agosti 31,mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ( Mwalimu Nyerere Memorial Hospital) iliyopo Kwangwa Manispaa ya Musoma watoto 21 wamezaliwa salama hospitalini hapo huku kinamama zaidi ya 50 pia wameweza kuhudumiwa ndani ya siku tatu, anaripoti AMOS LUFUNGULO-MARA.
Dkt.Eyembe ameyasema hayo leo mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine amebainisha kwamba, hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ni ya uhakika kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli kuimarisha sekta ya afya na hivyo kuwatendea haki Watanzania kwa vitendo.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambayo ni moja ya mradi wa kimkakati uliotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, kutaongeza fursa ya uchumi wa Mkoa wa Mara kwani wananchi kutoka Mkoa wa Mara, mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na nchi ya Kenya watafika kupatiwa huduma za matibabu hususan huduma ya kusafisha figo.
Huduma ambayo itakuwa ikitolewa kwa gharama ya shilingi 200,000 pamoja na huduma za kibingwa za upasuaji wa mifupa ambazo pia zitatolewa baada ya kitengo hicho kuanza kufanya kazi.
Akizungumzia kuhusiana na madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara pia Dkt.Eyembe amebainisha kwamba, mpaka sasa kuna madaktari wa kutosha ambao idadi yao ni 34, pamoja na madaktari bingwa wanne ambapo kati yao wawili ni madaktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, mmoja daktari bingwa wa magonjwa ya mifupa na daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dkt.Joachim Eyembe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo. PICHA NA AMOS LUFUNGULO/www.diramakini.co.tz |
Dkt.Eyembe ametoa shukurani kwa Rais Magufuli, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kwa namna ambavyo wamefanikisha ujenzi huo kukamilika kwani hospitali hiyo ilianza kujengwa miaka ya 1977 na ilikwama kukamilika hadi Serikali ya Awamu ya Tano ilipoinasua kwa kutoa fedha shilingi Bilioni 15 ambazo zimekamilika ujenzi huo.
Neema Mwita mkazi wa Kwangwa amesema, anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha hospitali hiyo na kutoa kipaumbele kwa kuanza kutolewa huduma ya mama na mtoto jambo ambalo amesema lina faida kwao, kwani watajifungua salama na kupatiwa huduma zingine kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Esta Matiko mkazi wa Kiara amesema, anashukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara chini ya Dkt.Eyembe kwa namna ambavyo wamekuwa wakitoa huduma kwa ubora na kwa weledi ikiwemo lugha nzuri za madaktari na wauguzi pamoja na kuhudumiwa kwa haraka amesema waendelee na moyo huo huo.