WAZIRI BITEKO:Habari kuwa Kampuni ya Madini ya Barrick Gold Corporation ilisaini Mkataba mwaka 2017 na kusaini mkataba mwingine mwaka 2020 si za kweli, wapuuzeni hao wapotoshaji

Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema taarifa zinazoenezwa kwenye vyombo vya habari kuwa Kampuni ya Madini ya Barrick Gold Corporation ilisaini Mkataba mwaka 2017 na kusaini mkataba mwingine mwaka 2020 si za kweli, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Waziri wa Madini,Mheshimiwa Doto Biteko
Waziri wa Madini Doto Biteko amefafanua kuwa Barrick ina mkataba mmoja tu uliosainiwa na Tanzania ambao ulisaiwa Septemba 24,mwaka huu.

Ameongeza kuwa, hakuna mkataba wowote uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Barrick Gold Corporation mwaka 2017 kama watu wanavyojaribu kupotosha umma.

Biteko amesema hayo mjini Geita wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambao walitaka kupata ufafanuzi kuhusu habari zilizoenezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusu Serikali na Kampuni ya Barrick kuwepo utata kwenye mikataba.

Kwa mujibu wa Doto Biteko Wizara ya Madini baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na majadiliano na kampuni hiyo, mabadiliko kadhaa yalifanyika katika mikataba na hadi sasa yanatekelezwa na kampuni husika.

Ametaja baadhi ya masharti kuwa ni kufungua akaunti za Barrick Gold Corporation ndani ya Tanzania jambo ambalo kampuni hiyo imetekeleza kwa vitendo.

Aidha,walikubaliana pia endapo kampuni hiyo imepata mkopo nje ya nchi ni lazima kusajiliwa hapa Tanzania kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kuhusu suala la kusafirisha Makinikia,Waziri ameeleza kuwa, zamani yalikuwa yanasafirishwa hadi eneo la kuyeyushia (smelting point), lakini kwa sasa mnunuzi analeta fedha Tanzania na kuja kununulia hapa nchini.

Ametaja Sekta ya Madini kuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi na kuleta mafanikio makubwa serikalini katika ukuaji wa kisekta,kuingiza fedha za kigeni nchi,kuongezeka mapato yanayotokana na madini kwa mwaka kulinganisha na sekta nyingine.

Ametaja Sekta ya Madini hadi sasa imekua kwa asilimia 17.7,imeongoza kwa kusafirisha bidhaa zote  nje ya nchi,sekta ya madini inasafirisha asilimia 51.9 na mapato kutokana na madini yameongezeka kwa mwaka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi Bilioni 520 kwa mwaka.

Waziri Biteko yuko mjini Geita akishuhudia maonyesho ya tatu ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika Kijiji Maalum cha maonyesho kilichoanzishwa katika Mtaa wa Bombambili mjini Geita chini ya ufadhili wa Mgodi wa Uchimbaji wa Dhahabu (GGML).

Afisa Mawasiliano wa GGML, Theophil Pima amesema kuwa, mgodi huo umetoa fedha kutoka kwenye mkakati wake wa kusaidia jamii(CSR) kiasi cha sh.milioni 800 kuanza ujenzi wa eneo la maonyesho.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel anasema kuwa, kijiji hicho kina ukubwa wa ekari 100 na kitakuwa na majengo mbalimbali ambapo sasa lipo jengo moja la utawala.

Baadhi ya huduma zitakazotolewa katika kijiji hicho ni pamoja na mabenki, burudani,kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimataifa, pamoja na eneo la kufugia wanyamapori kwa ajili ya utalii wa ndani.

Kukamilika kwa kijiji hicho cha maonyesho katika mji wa Geita itakuwa ni moja ya uwekezaji mkubwa kwa maendeleo ya mji wa Geita unaotokana na fedha za makampuni ya madini.

Mradi huo unatokana na fedha za CSR ambazo hupatikanaji wake umechagizwa kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ya sheria ya madini yaliyo fanyika mwaka 2017 ili kusimamia na kuelekeza Makampuni hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news