Waziri Hasunga azindua utoaji mikopo ya zana za kilimo, wakulima milioni 1.2 wasajiliwa

Katika kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora, mbolea na viatilifu kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya milipuko, anaripoti Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es Salaam.

Pia Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi.

Katika kufikia azma hiyo, Wizara ya Kilimo imeanzisha Kitengo cha Masoko ya Mazao (Agricultural Marketing Unit) katika Idara ya Maendeleo ya Mazao inayosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia/kusimamia mifumo ya uuzaji wa mazao.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo Septemba 22, 2020 wakati wa uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam. (Wizara ya Kilimo).
Sehemu ya wakulima na washiriki wa hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati wa hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela  akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga kwa ajili ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam.
Waziri wa Kilimo ,Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akiwasha trekta ishara ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza akimkabidhi trekta Yusuph Msafiri mkulima wa misitu kutoka Kilolo wakati wa uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na ETC Agro, LoanAgro na Agricom hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam.

Pamoja na hayo amesema kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma za bima ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti Shughuli za Bima nchini (TIRA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), kampuni binafsi tano (5) za bima zimeanzisha Bima ya Mazao kwa lengo la kumsadia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupata dhamana ya mikopo.

Kuhusu usajili wa wakulima,Waziri Hasunga amesema kuwa, Serikali imefanya zoezi la kuwatambua, kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wakulima. 

Zoezi hilo lilifanywa kupitia Bodi za Mazao. Hadi sasa, wakulima 1,279,884 wa mazao ya biashara wamesajiliwa na kutengeneza kanzidata au database kwa lengo la kuwatambua na kusaidia katika utoaji wa huduma za kilimo ikiwemo huduma ya bima ya mazao.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa LoanAgro Kashyap Godavarthi, Mkurugenzi Mtendaji wa ETC Agro, Shashi Gupta, Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom, Angelina Ngalula, Viongozi na Wafanyakazi wa Benki ya CRDB, ETC Agro na LoanAgro, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo na kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali.

Kadhalika, Hasunga ameipongeza benki hiyo kwa kuwa kinara wa uwezeshaji sekta ya kilimo ambapo takwimu zinaonyesha asilimia 40 ya mikopo yote ya kilimo nchini imetolewa na Benki ya CRDB.

Amesema kuwa, kilimo ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu kutokana na mchango wake katika uchumi. 

Takwimu zinaonyesha sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 28 katika Pato la Taifa, huku ikitoa ajira kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania.

Pia amesema kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo vinavyoweka mkazo kwenye mapinduzi ya viwanda, kwa pamoja vanaitambua Sekta ya Kilimo kama mhimili imara utakaowezesha upatikanaji wa malighafi za viwanda na kukuza uchumi wa taifa letu.

Waziri Hasunga amesema kuwa, takwimu zinaonesha ni asilimia nane ya mikopo yote iliyotolewa na taasisi za fedha katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilielekezwa katika sekta ya kilimo. Kiwango hicho kinajumuisha mikopo ya fedha pamoja na pembejeo za kilimo. Hiki ni kiwango kidogo ukilinganisha na umuhimu wa sekta hii katika uchumi wa taifa letu.

Hivyo basi, ili kuweza kufikia malengo serikali iliyojiwekea taasisi za fedha na wadau wengine wa sekta ya kilimo wanahitaji kuwekeza zaidi katika ubunifu wa huduma na bidhaa zenye vigezo na masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa, katika kuunga mkono juhudi za kuboresha kilimo nchini, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Benki ya CRDB imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika kilimo.

Amesema, Benki ya CRDB ndio inayoongoza nchini kwa kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa asilimia 40 ya mikopo yote ya kilimo nchini. "Kama unavyofahamu Mheshimiwa kuna taasisi za fedha zaidi ya 58 nchini na kwa ujumla wao wanatoa asilimia 60 wakati Benki ya CRDB pekee inatoa asilimia 40. Hii inadhihirisha adhma ya Benki ya CRDB ya kuunga juhudi za serikali za kuwaletea watanzania maendeleo kwa vitendo,"amesisitiza Nsekela.

Ameongeza kuwa, mikopo ya kilimo toka Benki ya CRDB imeelekezwa katika maeneo kama vile: Pembejeo na uendeshaji, Zana za kilimo Ujenzi wa maghala, Uunganishwaji na masoko, Uwekezaji kwenye viwanda, Elimu ya mambo ya fedha ili kutoa ufahamu wa uwekezaji na kuwajengea wakulima uwezo Ufugaji wa mifugo, nyuki na samaki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news