Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika akizungumza na watumishi na wananchi wilayani Ngorongoro kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.
WATANZANIA wameaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kuzitumia vizuri Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini ili kuwa chachu ya maendeleo kwenye jamii wanayoishi, ikizingatiwa kuwa rushwa ikishamiri katika taifa lolote lile huwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, anaripoti MARY MWAKAPENDA kutoka NGORONGORO.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Huruma Mkuchika wakati akiwasihi wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuitumia vizuri Ofisi ya TAKUKURU wilayani humo, aliyoizindua rasmi Septemba 4, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro ofisini kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Rashid Taka (wa kwanza kulia kwa Waziri) alipoitembelea ofisi hiyo kabla ya kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.
Mheshimiwa Mkuchika amesema, njia sahihi ya kuleta maendeleo nchini ni ushiriki wa kila Mtanzania kuwafichua wala rushwa na kutoshiriki vitendo vya rushwa, hususani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambao taifa linategemea kupata viongozi bora wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo.
"Msishawishike kuomba rushwa wala kupokea rushwa kwa lengo la kumchagua kiongozi wa chama chochote kile cha siasa,”Waziri Mkuchika amewaasa wananchi na kuongeza kuwa, uchaguzi ukighubikwa na vitendo vya rushwa hautakuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.
Baadhi ya watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu Mheshimiwa George Huruma Mkuchika (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU wilayani humo Septemba 4, 2020.
Aidha, kuhusu azma ya Serikali kuokoa fedha za umma, Mheshimiwa Mkuchika ameipongeza TAKUKURU Mkoa wa Arusha kwa kuokoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 2,490,396,226.00 katika kipindi cha mwaka 2019/2020, fedha ambazo zitatumika kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo.
"Kama mnavyofahamu mtazamo wa mataifa kwa sasa ni kurejesha serikalini mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa na ubadhirifu ili zitumike kwenye shughuli za maendeleo,"Waziri Mkuchika amefafanua.
Mheshimiwa Mkuchika ameahidi kuwa, Serikali itahakikisha TAKUKURU inaendelea kuimarika, hivyo amewataka watumishi wa TAKUKURU kuongeza juhudi katika kutekeleza jukumu lao la kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja akitoa maelezo ya awali kuhusu jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo Septemba 4, 2020.
Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa kuwajengea ofisi na kuwapatia rasilimali za kutosha, hivyo ameahidi kuwa TAKUKURU itafanya kazi kwa bidii kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Ufunguzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Ngorongoro ni ushahidi wa namna Serikali ilivyodhamiria kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuiwezesha TAKUKURU kuwa na ofisi itakayorahisisha utendaji kazi wake.Zinazofanana soma hapa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika akikata utepe kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 4, 2020. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Rashid Taka na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja.