Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Uokovu wa Wananchi ya Mali (NCSP), Kanali Assimi Goita amewahutubia wananchi kwa njia ya televisheni na kumtangaza, Ba N'Daou aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo kuwa Rais wa Serikali ya mpito ya Mali.
Ba N'Daou ameteuliwa na kikosi cha wanajeshi waliofanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keit mwezi Agosti 18, mwaka huu.
Kanali Assimi Goita ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais ambapo sherehe za kuwaapisha viongozi wote hao zimepangwa kufanyika Septemba 25, mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na mashinikizo ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).
Kamati ya Taifa ya Uokovu wa Wananchi ya Mali imeahidi kuheshimu makubaliano yote ya kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi yanayobeba silaha baada ya kupinduliwa Rais Boubacar Keita nchini humo.