Wizara ya Ardhi yazindua Siku Maalum ya Mlipakodi ya Ardhi

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua rasmi Siku Maalum ya Mlipa Kodi ya Pango la Ardhi itakayoendeshwa katika mikoa yote ya Tanzania,anaripoti Munir Shemweta, WANMM DODOMA.

Uzinduzi huo ambao ni mkakati maalum wa Wizara ya Ardhi kuhamasisha wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya pango la ardhi ambapo na utekelezaji wake ulianza mwishoni mwa wiki mkoani Dodoma kwa Maofisa Ardhi wa Makao Makuu kwa kushirikiana na wale wa ofisi za ardhi za mikoa na wa jiji la Dodoma kutembelea mitaa ya Kisasa na Ilazo.

Maafisa wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiangalia Ramani ya eneo la Kisasa katika jiji la Dodoma kabla ya kuanza zoezi la siku ya Mlipa Kodi ambapo walitembelea nyumba kwa nyumba kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi sambamba na kusikiliza changamoto za sekta ya ardhi mwishoni mwa wiki jijini Dodoma. (MUNIR SHEMWETA-WIZARA YA ARDHI).
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami, zoezi hilo la siku ya Mlipa Kodi ya Pango la Ardhi litakuwa likifanyika kila siku ya Ijumaa kwa Maafisa wote wa Ardhi nchi nzima kutembelea mitaa mbalimbali nyumba kwa nyumba kwa lengo la kutoa elimu na kutatua changamoto za ardhi.

‘’Zoezi hili litakuwa likifanyika kila siku ya Ijumaa na litahusisha maafisa wote wa ardhi katika mikoa ya Tanzania Bara na hapa Maafisa Ardhi hawatakiwi kujionesha wao ni nani kinachotakiwa ni kutoa elimu na leo tumeanza jiji la Dodoma kama uzinduzi rasmi wa siku hiyo,’amesema Denis Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi alisema, mbali na zoezi hilo la kutembelea wamiliki wa ardhi nyumba kwa nyumba kutatua changamoto za ardhi pia llitatumika kuhuisha kumbukumbu za ardhi kwa wamiliki na kukagua uendelezaji miji.

Masami amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanaacha mawasiliano sahihi majumbani mwao ili maofisa ardhi watakapopita na kuwakosa waweze kuwasiliana kwa njia ya simu ili kupata taarifa sahihi zitakazowezesha uhuishaji kumbukumbu za ardhi kwa wamiliki.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 ya kodi ya pango la ardhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news