WIZARA ya Fedha na Mipango imekanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa inashirikiana na Shirika binafsi la BACC kutoa mitaji ya biashara na kilimo bila riba wala vikwazo, anaripoti PETER HAULE, IVONA TUMSIME kutoka WFM.
Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma. |
Akiongea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja, amesema taarifa hiyo ipuuzwe kwa kuwa wizara ina utaratibu maalumu wa kufikisha taarifa kwa umma.
“Wizara hutumia njia rasmi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyosajiliwa na kutambulika na Serikali kutoa taarifa zake, hivyo ni vema kutambua kuwa wizara haihusiki katika taarifa hizo zenye lengo la kupotosha umma na kuibua sintofahamu miongoni mwa jamii,”amesema Mwaipaja.
Ameitaka jamii kujihadhari na genge hilo la matapeli wanaotumia mitandao ya kijamii kuwarubuni ili kujipatia fedha za wizi.
Amesema kuwa, wizara haitambui na wala haijawahi kujihusisha kwa namna yoyote na kampuni hiyo na wala wizara haina mradi wowote wa namna hiyo wa kuwakopesha wafanyabiashara na wakulima mikopo isiyo na riba wala vikwazo.“Hao ni matapeli wa kimtandao, wapuuzeni,”amesisitiza Bw.Mwaipaja.
Aidha, amewaonya watu wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja kwani wanatafutwa na vyombo vya dola kwa udi na uvumba na kwamba wakipatikana hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Bw. Mwaipaja amewataka wote ambao watapenda kupata maelezo ya ziada kuwasiliana na Kitengo cha Mawasilaiano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Namba ya simu ya mkononi 075481562.
��
ReplyDelete