Zaidi ya Shilingi Trilioni Moja zapelekwa mkoani Arusha kwa miradi ya maendeleo, Mrisho Gambo naye afunguka

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idi Kimanta amesema katika kipindi cha miaka mitano zaidi ya Shilingi Trilioni Moja zimepelekwa mkoani humo kwa ajili ya huduma na miradi ya maendeleo ikiwa ni kiasi kikubwa cha fedha zilizopelekwa tofauti na mikoa mingine nchini, anaripoti Pius Ntiga, Arusha.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM mjini Arusha.

Katika mahojiano hayo Kimanta amesema, kiasi hicho cha fedha kilichopelekwa mkoani humo kuanzia mwaka 2015-2020 ni kikubwa mno tofauti na mikoa mingine hivyo akampongeza Rais John Magufuli kwa upendo wake kwa wananchi wa Arusha.

Amesema, kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 500 zimetumika katika mradi mkubwa wa kimkakati wa maji utakaohudumia wananchi wa Mji wa Arusha na vitongoji vyake, ambao umeanza kunufaisha wananchi wa Arusha ambao wameupongeza.

Kimanta amesema, kila mwaka fedha za maendeleo zimekuwa zikiongezeka ambapo shilingi Bilioni 58 ni kwa ajili ya miradi ya barabara na Shilingi Bilioni 70 kwa ajili ya afya zimekuwa zikiufikia mkoa huo.

Pia Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha amesema, jumla ya Shilingi Milioni 900 zimepelekwa kwa ajili ya miradi mikubwa ukiwemo ule wa maji mkubwa Arusha na barabara ikiwemo ya Baypas.

Pamoja na mambo mengine amesema, elimu bure hadi sasa mkoa umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 170 kwa ajili ya elimu bure kwa shule za msingi na hali hiyo imeongeza hali ya ufaulu na idadi ya wanafunzi shuleni.

Amesema, idadi ya wanafunzi imeongezeka na kuleta changamoto ya idadi ya madarasa mkoani Arusha, ambayo wanaendelea nayo kuitafutia ufumbuzi.

Aidha, jumla ya Bilioni 6 amesema zimeletwa Arusha kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe ikiwemo Iriboru.

Pia amesema hospitali za wilaya zinajengwa na hivyo kufanya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kutekelezwa vizuri ikiwemo sekta ya utalii.

Kuhusu sekta ya utalii amesisitiza kwa sasa ipo vizuri licha ya janga la maambukizi ya virusi vya Corona kuukumba Mkoa wa Arusha na maeneo mengine nchini.

"Sekta ya Utalii ipo vizuri na inaiingizia pato zuri kwa Taifa na Mkoa wa Arusha kwa ujumla,"amesema Mkuu wa Mkoa.

Kuhusu hali ya ulimzi na usalama mkoani Arusha amesema, ni nzuri na amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimania vizuri hali ya ulinzi.

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi Mkuu, Kimanta amesema hadi sasa shughuli za kampeni zinaendelea vizuri kwa vyama vya siasa kuendelea kunadi sera zao katika mikutano ya kampeni ambayo inahudhuriwa kwa wingi na wananchi.

Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu kwani hali ya ulinzi umeimarishwa vizuri.

"Wananchi wanajitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano ya kampeni na wana matumaini kuwa Oktoba, 28 wananchi watajitokeza kwa wingi bila bughudha kwenda kupiga kura,"amesema Kimanta.

Kuhusu ujio we reli amesema,imeunufaisha Mkoa wa Arusha kupitia treni ambayo ilisimama zaidi ya miaka 30 umri ambao ni wa mtu nzima.

"Mwezi iliyopita Mkoa wa Arusha ukipata treni ya kwanza ya mizigo baadye treni ya abiria ambayo itachochea huduma za ukuaji wa uchumi wa wananchi na mkoa kwa ujumla,"amesema.

Amesema, treni ya kwanza ilileta mzigo ambao ungebebwa na malori zaidi ya 80, lakini ukaletwa na treni na hatua hiyo imepokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa Arusha.

Kuhusu vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli vimechochea ukuaji wa uchumi na pato la wananchi wa Arusha kwani kwa sasa wafanyabiashara wadogo hawazipati tena kero jijini Arusha.

Amesema wafanyabiashara hao sasa wanafanya shughuli zao vizuri bila vitisho vyovyote na kwamba Shilingi Bilioni 22 za makusanyo ya mkoa tangu 2015 hadi sasa ni ongezeko la asilimia 53 yaani mara mbili umeongezeka ukiwemo mchango wa wafanyabiashara wadogo.

"Matarajio ya Wana Arusha 2020-2025 ni makubwa na watarajie Arusha itapaa zaidi tofauti na ilivyo sasa na watatoa Asante Oktoba 28, mwaka huu,"amesema Kimata.

Pia Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha amewata wananchi watunze kadi zao za kumpigia kura na wakapige bila wasiwani wowote kwani hali ya ulinzi imeimarishwa na baada ya Uchaguzi Mkuu jijini Arusha.

Amewataka pia viongozi wa vyama vya siasa wafanye kampeni kwa staha na watumie lugha ambazo hazitaleta chuki kwa wananchi.

Wakati huo huo, Mgombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mrisho Gambo, amewataka wananchi kuzipuuza ahadi zinazotolewa na wanasiasa wa upinzani akiwemo Godbless Lema ambaye amedai yupo kwenye harakati za kuaga kwani hana chake tena Oktoba 28, mwaka huu.

Amesema, utendaji kazi wake uliotukuka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha unampa jeuri ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani aliwatumikia kwa moyo wake wote wana Arusha.

"Nawaomba kura zenu wananchi wa Arusha Mjini Oktoba 28, mnichague kwa kura nyingi ili tuendeleze maendeleo ya Arusha,"amesema Gambo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news