Zanzibar kufanya maboresho makubwa sekta ya afya

WIZARA ya Afya Zanzibar inatarajia kuzindua Mpango Mkakati wa Kidigitali wa Sekta ya Afya utakaoweka mifumo bora ya uimarishaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar kuanzia mwaka huu, anaripoti RAMADHANI ALI kutoka MAELEZO ZANZIBAR.
Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma akitoa taarifa kuhusu uzinduzi wa mpango mkakati wa Kidigitali wa Afya unaotarajiwa kuzinduliwa Septemba 10,mwaka huu.

Mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Afya,Hamad Rashid Muhamed kesho katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni.

Akizungumza na waandishi wa habari,Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Afya, Ramadhani Khamis Juma amesema,mpango huo wa miaka mitano utapunguza gharama kwa Serikali na wagonjwa.

Ameweka wazi kuwa mpango huo utaimarisha upatikanaji wa huduma na utarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa ambazo zitasaidia uongozi wa wizara kutoa maamuzi yaliyo sahihi ya afya katika wakati mwafaka.

Aidha,amesema mpango huo wa kidigitali utaweka kumbukumbu zote muhimu za wagonjwa watakaofika hospitali kupata huduma kwa njia ya kdiijitali kutoka hospitali na vituo vyote vya afya.

Amewahakikisha wananchi kuwa Serikali imejipanga kikamilifu na wana uhakika kuwa, mpango huo utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya,Mwinyi Msellem alieleza kuwa Mpango Mkakati wa Huduma za Afya Zanzibar, utasaidia kulinda maadili na utaongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wagonjwa.

Amesema, baada ya kumalizika kipindi cha miaka mitano mpango huo utafanyiwa mapitio ili ikionekana kulikuwa na mapungufu katika utekelezaji yaweze kufanyiwa kazi.

Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Wizara ya Afya, Mohamed Habib amesema, mpango huo pia utasaidia sekta nyingine muhimu za Serikali ikiwemo sekta ya elimu.

Aidha,amesema katika kuhakikisha mpango huo unakuwa wa mafanikio, wameandaa mifumo mbadala ya upatikanaji wa miundombinu ya dharura ikiwemo huduma ya umeme na mitandao ya simu.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Mwinyi Msellem akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Mpango Mkakati wa wa Kidijitali wa Afya Zanzibar. (Picha na Makame Mshenga).



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news