Zanzibar ni moja wapo ya vituo vitakavyonufaika na ushirika wa Emirates na flydubai kupitia usafirishaji

KUFUATIA kuendelea kurejea kwa safari za ndege za abiria, mashirika mawili makubwa ya ndege za Kimataifa ya Emirates na flydubai yamefufua ushirikiano wao uliofanikiwa na wa kimkakati ili kuweza kuwahudumia wateja wao kwa urahisi na kwa ufanisi mkubwa duniani, anaripoti MWANDISHI WETU, www.diramakini.co.tz.

Wateja wa Emirates sasa wanaweza kusafiri kwenda zaidi ya vituo 30 vinavyohudumiwa na flydubai, wakati wateja wa flydubai wana uwezo wa kupata huduma zaidi ya vituo 70 kupitia ndege za Emirates.

Baadhi ya vituo vya flydubai vitakavyohudumia abiria wa Emirates ni pamoja na Zanzibar, Belgrade, Bucharest, Kyiv, and Sofia.
Ushirikano huo kati ya Emirates na Flydubai ulianza Oktoba, 2017 na kupokewa vema na wateja ambao waliweza kufaidika na muungano huo ambao uliwapa fursa ya kuchagua aina ya safari wanayotaka kupitia mashirika hayo makubwa ya Dubai.

Zaidi ya abiria milioni 5 walinufaika na ushirikiano huo ambapo walikuwa wanahudumiwa katika safari na majiji tofauti katika miaka miwili ya ushirikiano.

Akizungumzia juu ya kurejewa upya kwa ushirika huo, Adnan Kazim, Afisa Mkuu wa Biashara wa Emirates amesema, "Tunafurahi kutangaza kwamba wateja wetu wanaweza kutumia fursa ya ushirikiano huu kati ya sisi Emirates na Flydubai kupata huduma bora katika mtandao ulioimarishwa wa miji kwa tiketi moja na huu ni mpango uliozingatia uaminifu, salama, kuwapa furaha na wenye kuwapa faraja kupitia Dubai na mizigo yao itakuwa salama hadi mwisho wa safari,"amesema.

Naye Hamad Obaidalla, Afisa Mkuu wa Biashara kutoka flydubai amesema, "Tuna hakika kwamba mahitaji ya kusafiri yataendelea kuongezeka wakati nchi nyingi zinaanza kuondoa vizuizi katika safari za Kimataifa. Flydubai imeanzisha tena usafirishaji hadi vituo 32 karibu na mtandao tangu Juni na tunatarajia idadi hiyo itaongezeka kwa kasi katika miezi michache ijayo.

Dubai imeweka itifaki madhubuti za kiafya na usalama ambazo zinawapa nafasi abiria wanaosafiri iwe kwa biashara, burudani au kuungana tena na wapendwa wao.

"Tunaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha safari zetu ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali kupitia usafiri wa anga kutoka na kuingia na kuongeza shughuli za kubeba mizigo. Ushirikiano wetu na Emirates utaendelea kuwezesha mtiririko zaidi wa abiria na mizigo katika mitandao yetu ya pamoja,"amebainisha Obaidalla.

Emirates na flydubai ambazo zina uzoefu mkubwa wa safari za Kimataifa zimedhamiria kuendelea kudumisha vipaumbele vyake ambavyo ni usalama na afya za wateja na wafanyakazi wawapo ardhini na angani kama kipaumbele chao cha juu.

Mashirika hayo mawili kila moja limetekeleza kwa ufanisi hatua kubwa za usalama katika kupambana dhidi ya mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) katika kila hatua ya safari ya mteja pamoja na usafi ulioimarishwa wa vituo vyote ikiwemo ndani na nje ya ndege ili kuondoa vumbi na aina nyingine za bakteria.

Wateja wanaopita kupitia Dubai hupitia uchunguzi wa joto kwenye uwanja wa ndege. Pia maeneo ya kupitia katika uwanja wa ndege wa Dubai yamewekwa mashine maalum za kinga dhidi ya vijidudu na wafanyakazi wa uwanja wa ndege waliovaa vifaa kinga vya kibinafsi (PPE) wanapatikana ili kutoa msaada zaidi.

Ndege kadhaa za flydubai huwa zinafanya safari zake katika vituo vilivyopo barani Afrika, Asia ya Kati na Ulaya zinafanya kazi kutoka Terminal 3 ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, na kuwezesha uhusiano mzuri kwa abiria wanaosafiri kwa ndege za Emirates kwenda na kutoka Dubai.Unaweza kusoma zaidi kuhusu safari za Emirates hapa.

Uchunguzi wa COVID-19 PCR ni lazima kwa wateja wote wanaoingia na kusafiri kwenda Dubai,lengo likiwa ni kuhakikisha usalama wakati wa kutoka au kuingia uwanja wa ndege kwa wateja wa Emirates na Flydubai.

Wateja wanaopanda ndege za Emirates pia watapewa bure vifaa vya usafi ikiwemo barakoa, mipira ya kuvaa mikononi, vitakasa mikono na dawa ya kudhibiti bakteria.

Mnamo Agosti 2018, flydubai iliipitisha Emirates Skywards kama mpango wake wa uaminifu, ikiruhusu wateja kupata zaidi Skywards Miles na Tier Miles ambao ni utaratibu unaowawezesha wadau wao kupata upendeleo maalum na fursa nyingi kulingana na viwango vya uanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news