Zanzibar yaendelea kuandikisha mafanikio ya kihistoria kupitia Rais Dkt.Shein

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba ilifanya juhudi za makusudi katika kulibadilisha zao la karafuu kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) ili liende na wakati uliopo.

Ameyasema hayo leo Septemba 17, 2020 katika ufunguzi wa kiwanda cha kusarifu majani makavu na yaliyoanguka yenyewe ya karafuu, huko Mgelema Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ambacho kimejengwa kwa ushirikiano na Shirika la ZSTC pamoja na Kampuni ya Indesso kutoka nchini Indonesia.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, kwa sasa Shirika la ZSTC linakwenda kwa mabadiliko ya biashara na matumaini yake ni kwamba Awamu ya Nane ijayo itayaendeleza.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Saba iliongeza bei za zao la karafuu kutoka sh.3,500 hadi kufikia sh.14,000 huku ikisisitiza kuwa, hata soko la Dunia likishuka basi Serikali itaendelea kuwalipa wakulima kwa bei hiyo hiyo ambayo inayoendela hadi leo.

Ameongeza kuwa, uwekezaji huo ni uhusiano na ushirikiano mwema kati ya Zanzibar na Indonesia.

Amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kujenga kiwanda hicho kwa lengo la kufahamu kuwa Mgelema na Ngomeni ni nguzo kubwa ya uzalishaji wa zao la karafauu.

Rais, Dkt.Shein amesema kuwa, katika kuhakikisha uimarishaji wa zao la karafuu pamoja na bidhaa zake zinaimarika katika eneo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kazi ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Amesema kuwa, tayari Serikali imeshajenga barabara ya Ngomeni pamoja na kupeleka kituo cha afya, umeme pamoja na huduma nyingine hivyo, baada ya miezi miwili barabara ya kutoka Kipapo hadi Mgelema itajengwa na kuahidi kuwa maisha ya wananchi wa kijiji hicho yatabadilika.

Aidha, Rais Dkt.Shein ametumia fursa hiyo kutoa historia fupi ya zao la karafuu pamoja na biashara yake kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 na baada ya Mapinduzi hayo.

Katika maelezo yake hayo, Rais Dkt.Shein ameeleza kuwa, wananchi wa Zanzibar ndio waliopanda mikarafuu lakini wao hawakunufaika na zao hilo na badala yake walinufaika watawala waliotoka nje kuja kuitawala Zanzibar.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Shein ameeleza kuwa bado karafuu ya Zanzibar inatakiwa na inapendwa kwani bado soko lake lipo na tayari hivi sasa karafuu imerudi hadhi yake ambapo hata magendo ya karafuu yamepungua kwa asilmia tano na kuonesha wazi kuwa hayapo.

Amesisitiza kuwa, jumla ya tani 33,549.8 za karafuu kavu zenye thamani ya sh.Bilioni 448.684 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019 na jumla ya tani za karafuu 32,142.17 zenye thamani ya dola za Kimarekani 297,707,844 sawa na sh. Bilioni 553.89 zimeuzwa nje ya nchi.

Rais Dkt.Shein ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka tisa mfululizo Serikali ilimpa mkulimma kiwango cha asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la dunia ambayo ni sawa na sh.14,000 kwa kilo moja ya karafuu kavu za daraja ka kwanza.

Naye Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali amesema kuwa, kiwanda hicho kitachangia kwa kiasi kikubwa kipato kwa wananchi hasa vijana kwani ndio wanaojishughulisha kwa kiasi kikubwa na shughuli za kiwanda hicho.

Balozi Amina ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt.Shein kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kiwanda hicho ambacho kimetokana na ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Indonesia mnamo mwezi wa April mwaka 2018.

Akitoa taarifa za kitaalamu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Hassan Reli amesema kuwa, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kusindika kilogramu 250 za majani makavu kwa wakati mmoja na kutoa lita 7 za mafuta ambapo kitakuwa kikifanya kazi kwa muda wa saa 24 na hivyo kuwezesha kupatikana lita 21 za mafuta kwa siku.

Mapema Balozi wa Indonesia Dkt.Ratlan Pardede alisema kuwa, uzinduzi wa kiwanda hicho unaonesha uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia.

Ameeleza kuwa, tayari kwianda hicho kimeshaanza kuzalisha mafuta ya majani ya karafuu na kusisitiza kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni wa mwanzo tu na badala yake viwanda hivyo vitaendelea kujengwa Unguja na Pemba.

Amesema kuwa, kuanzishwa kwa kwianda hicho kunajumuisha uhamasishaji wa teknolojia na kufungua uwezekano mwingine katika sekta nyingine.

Mwakilishi wa Kampuni ya Indesso kutoka Indonesia Feri Augusta ametoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mzuri aliopata na kusisitiza kuwa, kampuni yake itaendeleza kiwanda hicho sambamba na kuanzisha vingine kwa manufaa ya nchi pamoja na wananchi hasa wale wanaokaa katika maeneo wanayoishi.

Mkuu wa kampuni hiyo akitoa salamu kupitia video maalum akiwa nchini Indonesia amema kuwa, kampuni yake itaendelea kutoa ushirikiano wake na Zanzibar kwani inathamini uhusiano uliopo pamoja na juhudi za Rais Dkt. Shein anazozichukua.Amesema kuwa, anathamani ushirikiano wa pamoja uliopo ambao yaliimarika zaidi pale Rais Dkt.Shein alipofanya ziara yake ya kiserikali nchini humo.

Katika uzinduzi huo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi mbalimbali.
Uzinduzi huo umepambwa na ngoma mbalimbali kutoka kwa wasanii wa kiwani Pemba ikiwemo ngoma ya kibati pamoja na burudani nzuri ya nyimbo za Indonesia iliyotumbuizwa na Putri Marsha Amanda na mwenzake Ni Waga Supriani kutoka Bali, nchini Indonesia na nyimbo yao hiyo ya utamaduni maarufu ya Puspanjali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news