"Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofauti zetu, ushindi huu ni wa wana CCM wote, wajibu ulio mbele yetu ni kudumisha amani yetu, mshikamano wetu na umoja wetu, uchaguzi sasa umekwisha turudi kuwa kitu kimoja,"Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mteule wa Zanzibar.
Dkt. Hussein Mwinyi ambaye alikuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa Rais mteule Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Dkt.Mwinyi amepata asilimia 76.27 ya kura hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa leo Oktoba 29,2020 jijini Zanzibar na Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Mkuu msaatfu Hamid Mahmoud Hamid.
Jaji Hamid amesema, Dkt. Mwinyi amepata kura 383,402 sawa na asilimia 76.27, hivyo kwa matokeo hayo amemtangaza Dkt. Hussein Mwinyi kuwa ndiye amechaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia sasa.
Amesema kuwa, kwa upande mgombea wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amepata asilimia 19.85 ya kura zote zilizopigwa. Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi wa matokeo ya kura zilizopigwa jana amemshukuru Mungu kwa kuwafikisha kwenye hatua ya kutangazwa rais wa Zanzibar.
Dkt.Mwinyi amesema, ameyapokea na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo na amepokea ridhaa ya Wanzibar na amewashukuru kwa kumwamini.
Pia amepongeza wagombea wengine na kwamba amejifunza mambo mengi kutoka kwao huku akibainisha kuwa, Zanzibar mpya itajengwa na wao wote na yupo tayari kuendeleza maridhiano yaliyopo kwenye katiba huku akisisitiza Zanzibar ni kubwa kuliko kitu chochote.
Tags
Habari