Walimu wanne akiwemo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chabutwa wilayani Sikonge mkoani Tabora wanashikiliwa kwa kosa la kujihusisha na wizi wa mitihani ya darasa la saba iliyomalizika jana nchini kote,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tabora, Mussa Chaulo amewataja walimu waliokamatwa kuwa ni Halima Joachim Kamilius, Ng’walu Biura Ndaturu wote kutoka Shule ya Msingi Chabutwa.
Pia Mkuu huyo wa TAKUKURU amemtaja Nyerembe Michael Kikudo wa Shule ya Msingi Sikonge aliyekuwa msimamizi wa mitihani ya jana.
Amesema kuwa,Mwalimu Mashaka Mwang’omo yeye anatuhumiwa kutoa rushwa ya sh 80,000 kwa msimamizi wa mitihani hiyo Mwalimu Nyerembe ili kumshawishi atoe nje ya chumba cha mtihani maswali ya mtihani wa sayansi uliokuwa ukiendelea wakati huo shuleni hapo.
Mkuu huyo amesema,uchunguzi wa makachero wao umebaini kuwa, karatasi ya maswali ya mtihani wa somo la sayansi ulitolewa nje ya chumba cha mtihani na kukamatwa kwenye chumba kisicho cha mtihani shuleni hapo. Amesema, katika chumba hicho ambacho hakikuwa na wanafunzi walikamatwa walimu wawili ambao ni Halima Joachim na Ng’walu Biura ambao walikuwa na mitihani.
Pia ameongeza kuwa, walimu hao walikamatwa wakiwa na tayari wameshajibu swali la 1 hadi la 8 na majibu yalikuwa yameandikwa kwenye plain paper na uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na utakapokamilika watauhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria huku akiwataka watumishi wengine kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu.
Tags
Habari