Dkt.Magufuli apiga simu kuwaomba kura wana Ushetu, Majaliwa asema anayo rekodi nzuri ya kufanya kazi

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amepiga simu na kuwaomba wakazi wa Ushetu wampigie kura za kutosha ili awatumikie. Ameongea nao leo jioni Oktoba Mosi, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Ushetu kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamilangano, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mgombea urais kupitia CCM, Dkt.John Magufuli wakati akiomba kura leo kwa wana Ushetu. (Diramakini).


“Watu wa Ushetu ninawashukuru sana kwa kumpitisha bila kupingwa Engineer Kuandikwa. Mimi niko Tunduma, nilitamani niwe hapo na ninyi lakini nimemtuma Waziri Mkuu aje kuniombea kura. Yote ambayo atazungumza Majaliwa nimemtuma mimi, nawatakia mkutano mwema,” amesema.

Amesema, ahadi yake aliyoitoa ya kutengeneza barabara ya Ushetu-Kahama iko palepale na kwamba akimaliza uchaguzi atafika kuwatembelea. “Naikumbuka hiyo barabara ya Ushetu kwenda Kahama, tutaitengeneza kwa kiwango cha lami. Naomba kura zenu pamoja na madiwani wote wa CCM.”

Baada ya Rais Dk. Magufuli kuzungumza na wananchi, Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wakazi hao wamchague kwa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani wa CCM.

Kwa upande wake, Eng. Kwandikwa alisema wananchi wa Ushetu wamepata mafanikio chini ya Rais Dk. Magufuli akitoa mfano wa ujenzi wa barabara za wilaya zilizojengwa kwa kiwango cha lami kilomita 1200 kutoka kilomita 400 mwaka 2015.

Pia alisema serikali ya awamu ya tano imeweka umeme katika vijiji 58 kati ya 112 na vilivyobaki vitapatiwa umeme. Kuhusu elimu, Eng. Kwandikwa alisema wamepokea sh. bilioni tano kwa shule za msingi, sekondari na miradi ya maji inaendelea katika wilaya hiyo.

Eng. Kwandikwa aliwataka wananchi wa Ushetu wamchague Rais Dk. Magufuli ili awaletee maendeleo katika nyanja mbalimbali zikiwemo huduma za afya, umeme, maji na barabara.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Geita yuko Mkoa wa Shinyanga akiendelea kutafuta kura katika wilaya mbalimbali.

MAJALIWA: DKT. MAGUFULI ANAYO REKODI NZURI YA KUFANYA KAZI, TUMPE NCHI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Bukombe, mkoani Geita wamchague Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu wanamjua historia yake na anayo rekodi nzuri ya kufanya kazi.

"Dkt. Magufuli tunamjua. Alikuwa Waziri katika nchi hii kwa miaka 20. Alikuwa Waziri wa Ujenzi akajenga barabara ambazo sote leo tunaziona. Alipoenda Wizara ya Ardhi, akapiga marufuku ya watumishi wa Wizara hiyo kujilimbikizia viwanja vinne vinne.”

Ametoa wito huo leo Oktoba Mosi, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Ushirombo katika mkutano uliofanyika kata ya Igulwa, wilayani Bukombe.

"Nimekuja kuwaomba kura zenu. Ni lazima tumpe kura mtu ambaye tunaijua historia yake ya kwamba aliwahi kuwa kiongozi na ameweka historia."

Amewataka wananchi hao wamchague kiongozi ambaye anaweza kuisimamia Serikali yake. "Usipokuwa makini unaweza kumpa mtu nchi halafu akashindwa kuisimamia nchi. Kiongozi anayefaa, mwenye uwezo wa kuratibu rasilmali zetu na kuzisimamia, si mwingine bali ni Dkt. Magufuli."

Amehimiza wakazi hao wawachague wagombea wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja. "Ni muhimu tuwe na madiwani ili waunde Baraza lao la Madiwani, waongee lugha moja na wapeleke hoja zao kwa Mbunge wao."

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Bukombe, Bw. Dotto Biteko na mgombea udiwani wa kata ya Igulwa, Bw. Richard Mabenga.

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe, kwenye mkutano wa kampeni, Oktoba 1, 2020. Katikati ni Mgombea Udiwani Kata ya Igulwa, Richard Mabenga. (PMO).

"Dkt. Magufuli amekuwa Rais kwa miaka mitano, aliyoyafanya katika kipindi kifupi tunayaona. Dkt. Magufuli huyu, wala rushwa ndiye kiboko yao. Leo niko mbele yako, bila kujali chama chako cha siasa, ninakuomba umpigie kura Dkt. Magufuli. Niko mbele yenu, ninawaomba kura za wagombea wa CCM," amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema wilaya ya Mbogwe imetengewa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Wilaya hiyo.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kabanga – Nhomolwa ambao ulipatiwa sh. bilioni 1.2. “Fedha nyingine zilizotolewa ni shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Mbogwe ambao utanufaisha maeneo ya Kasosobe, Bwelwa na Iboya.”

Amesema upanuzi wa mradi wa maji Nyakafuru umepatiwa sh. milioni 633 ambao utanufaisha maeneo ya Lulembela na Nyakafuru, Shinyanga A & B pamoja na usimikaji wa nguzo za umeme huko Nyakafuru, Shenda na Masumbwe.

Mheshimiwa Majaliwa amemaliza ziara yake mkoani Geita na anaendelea kutafuta kura katika Mkoa wa Shinyanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news