ELIMU YA MLIPA KODI NYUMBA KWA NYUMBA YATAJWA KUWA MWAROBAINI MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

Siku ya elimu ya mlipa kodi ya pango la ardhi imetajwa kuwa mwarobaini katika utatuzi wa migogoro ra ardhi hasa migogoro inayohusiana na mipaka ya viwanja pamoja na ile ya upimaji,anaripoti Eliafile Solla (WANMM) Manyara.

Hayo yamesemwa na Kaimu kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara, Bw.Leonardd Msafiri alipokutana na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ya pango la ardhi pamoja na masuala mengine yahusuyo sekta ya ardhi katika Mkoa wa Manyara.

Wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu nyumba kwa nyumba katika mtaa wa Negamsi (kwa Masista) Halmashauri ya Mji wa Babati.
Akizungumza katika utekelezaji wa zoezi hilo la utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba, Msafiri amesema wizara iligatua madara kwa maana ya kusogeza huduma karibu na mteja kutoka kuwa na ofisi za ardhi za kanda ambazo zilikuwa nane nchi nzima na kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kwenye kila mkoa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Msafiri amesisitiza kwamba, wizara imepiga hatua kubwa kuanzisha kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi kwa sababu utoaji elimu nyumba kwa nyumba unawapa fursa ya kukutana na wateja wao moja kwa moja na pia wanagundua changamoto nyingi na tofauti tofauti wanazokutana nazo wananchi katika maeneo wanayomiliki.

Mchungaji James Chimbalambala (wa pili kulia) akitoa historia ya kiwanja chake kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika mtaa wa Mji Mpya eneo la Kanisani Halmashauri ya Mji wa Babati, wakati wa utekezaji zoezi la elimu ya kodi ya pango la ardhi nyumba kwa nyumba.

Watendaji wa Sekta ya Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi makao makuu Dodoma, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara na Halmashauri ya Mji wa Babati wakipita nyumba hadi nyumba katika mtaa wa Negamsi kutoa elimu ya kodi ya pango la ardhi.

Baadhi ya watoa elimu ya mlipa kodi nyumba kwa nyumba kutoka Wizara ya Ardhi makao makuu Dodoma kwa kushirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu na ankara za madeni kwa wananchi wa mtaa wa Ngarenaro Halmashauri ya Babati Mji.
Nae Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi Makao makuu Dodoma, Bw.Denis Masami amesema, jukumu la msingi la wizara ni kupanga na kupima lakini hakuna upangaji wala upimaji utakaokuwa na tija kama wananchi watakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kupimiwa na kupangiwa maeneo yao.

Masami amesema kwamba, elimu inayotolewa sasa nyumba kwa nyumba ni fursa nzuri ya kuboresha kumbukumbu za wamiliki kutokana na uhalisia kwamba wizara imeboresha taratibu nyingi za utoaji hudumu zikiwemo zile za ukadiriaji kodi ya pango la Ardhi na ulipaji ambapo sasa zinafanyika kielektroniki.

Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara, Bw.Leonard Msafiri akiongea na kikosi kazi maalum cha kutoa elimu ya kodi ya pango la ardhi nyumba kwa nyumba kabla ya kuingia mitaani kutekeleza zoezi hilo.

Wataalam kutoka Wizara ya Ardhi makao makuu Dodoma, Halmashauri ya Mji wa Babati na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu kwa mkazi wa Mtaa wa Mji Mpya katika utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba.
Aidha, Zuberi Njola mkazi wa Mtaa wa Negamsi katika Halmashauri ya Mji wa Babati, ambaye alifikiwa na watoa huduma katika mji wake alifurahia sana zoezi hilo na kuiomba wizara kuwafikia wengi zaidi.

"Huu ni mkakati mzuri, tulio wengi hatuzijui haki zetu za msingi hasa kuhusiana na masuala ya ardhi. Pia migogoro mingi tunaitengeneza wenyewe kwa sababu hatuna uelewa wa mambo. Kutoa elimu nyumba kwa nyumba kama hivi kunaleta faraja kwetu wananchi, tunaiomba wizara iendeleze mkakati huu kwani tukishirikiana hakutakuwa na migogoro,"amesema Zuberi.

Siku ya elimu ya mlipa kodi ya ardhi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi ambapo kila siku ya Ijumaa watendaji wa sekta ya ardhi kote nchini hupita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kutoa elimu kwa wamiliki wa ardhi kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya ardhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news