IGP Sirro: Msituchokoze, tutawashughulikia wote mlioandaliwa kufanya vurugu

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limebaini kuna baadhi ya watu ambao wameandaliwa na viongozi wa kisiasa kwa ajili ya kufanya vurugu kipindi hiki cha uchaguzi na wengine kujikita katika uhalifu,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mkuu wa jeshi hilo, IGP Simon Sirro amesema watu hao bora waachane na mawazo hayo mara moja kwani jeshi lipo imara muda wowote pia amesema hadi sasa wananchi wengi wamekuwa watulivu.

Amesema hayo leo Oktoba 9, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Jiji la biashara Dar es Salaam huku akiwataka baadhi ya viongozi kujielekeza katika kunadi sera badala ya kuwatumia vijana kuwaingia katika masuala ya uhalifu.

Amesema, Jeshi la Polisi nchini limejipanga kikamilifu na yeyote ambaye atabainika kujihusisha katika uhalifu huo, mara moja atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Wakati huo huo amesema,wakati wa upigaji kura visiwani Zanzibar kuna baadhi ya watu au makundi ya watu yanahamasisha uvunjifu wa amani wakati wa zoezi hilo, huku akiwataka wananchi kuwapuuza kwa kuwa jeshi lipo macho saa 24 na hakuna ambaye atafanikisha mipango hiyo mibaya.

"Wananchi wetu wamekuwa watulivu sana, mpaka sasa tunakwenda vizuri katika kipindi hiki cha kampeni, ndiyo maana huko Tarime tumekamata vijana ambao wanapelekwa kwa ajili ya kufanya uhalifu, wanasiasa pambaneni na mambo ya siasa acheni kuwatumia vijana kuwaingiza kwenye uhalifu, wanapata shida wakati ninyi mnapata faida.Uhalifu hauwezi kukufanya ukawa kiongozi, sheria zipo na taratibu zipo, zifuatwe,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news