Joseph Kamonga asema atawatumikia wananchi wote Ludewa bila ubaguzi asisitiza maendeleo

Mbunge mteule wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema atawatumikia wananchi wote wa jimbo hilo bila ubaguzi wowote sambamba na kuwaletea maendeleo kulingana na uhitaji wao kwakuwa tayari anazifahamu changamoto zote za maeneo mbalimbali ya jimbo hilo,anaripoti Damian Kunambi (Diramakini), Njombe.
Hayo ameyasema wakati akikabidhiwa cheti cha ushindi wa kuwa mbunge wa jimbo hilo ambapo amekabidhiwa na msimamizi wa uchaguzi, Sunday Deogratius katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha kampeni amezunguka katika kata zote 26 za jimbo hilo pamoja na vijiji vyake 77 huku akiwa amefanya jumla ya mikutano zaidi ya 86 ikiwa ni ya kumuombea kura Rais John Pombe Magufuli pamoja na madiwani wa kata 11 zilizokuwa na upinzani.

"Kuzunguka katika maeneo yote haya ya jimbo langu kumenisaidia kuzijua changamoto za wananchi wangu pamoja na vipaumbele vyao hivyo kutokana na hilo mpaka sasa nimeshajua ni wapi pa kuanzia katika kuleta maendeleo wanayoyahitaji ,"amesema Kamonga.

Aidha, sambamba na kumkabidhi cheti hicho msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo amesema jimbo hilo kulikuwa na vituo 258 vya kupigia kura na matokeo ya vituo vyote hivyo kwa ngazi ya udiwani tayari yamekwisha ingizwa kwenye rekodi zao.

Amesema, matokeo ya ngazi ya udiwani katika kata 11 ambazo zilikuwa zikishindaniwa CCM imechukua kata 8 ambazo ni Manda, Nkomang'ombe, Ludewa, Mlangali, Madilu, Lifuma, Makonde pamoja na Kilondo huku CHADEMA wakichukua kata mbili ambazo ni Lupingu na Lumbila na ACT kata moja ambayo ni Luhuhu.

Ameongeza kuwa, madiwani wa kata nyingine 15 walipita bila kupingwa kupitia Chama Cha Mapinduzi na kupelekea kubakia kata 11 kati ya kata zote 26 za jimbo hilo.

Naye Katibu wa CCM wilayani humo, Bakari Mfaume amesema Joseph Kamonga si kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi bali ni kiongozi wa watu wote hivyo wapinzani wanapaswa kuonyesha ushirikiano wao kwa mbunge huyo mteule.

Amesema, mbunge huyo ana uwezo wa kuliongoza na kuleta maendeleo katika hivyo wananchi pamoja na wapinzani wanapaswa kumuamini kama alivyomuamini kwa kuteuliwa kuwa kamishna msaidizi wa ardhi katika jiji la Dodoma.

"Kamonga kutokana na uaminifu wake na kujituma katika kazi kulimfanya kuwa kamishna msaidizi wa ardhi katika jiji la Dodoma, lakini pamoja na kupewa wadhifa huo mkubwa kwa kuwajali Wanaludewa aliacha cheo chake na kuamua kuja kuwatumikia wananchi wa Ludewa hivyo kwa jambo hili tunapaswa kumpenda kama ambavyo yeye ametupenda,"amesema Mfaume.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news