Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (Korea Kaskazini), Kim Jong-un amesema Taifa lake litaendelea kujiimarisha katika masuala ya nyuklia na yeyote ambaye atawachokoza wapo tayari kutoa majibu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Picha iliyopigwa katika Shirika la Habari la KCNA wakati likirusha matangazo ya moja kwa moja, Kim Jong-un akihutubia baada ya kukagua gwaride kubwa la kijeshi.(KCNA VIA KNS/AFP/Getty Image). |
Jong -un ameyasema hayo katika hotuba ambayo inaelezwa kuwa ilikuwa nadra sana kwa leo Oktoba 10,2020 wakati akihutubia wananchi baada ya kukagua gwaride la kijeshi katika maadhimisho ya miaka 75 ya chama tawala.
Amesema, taifa lake lipo imara katika masuala ya kinyukilia na karibuni watazindua makombora mapya yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia na yanayoenda masafa marefu zaidi duniani.
Katika hafla hiyo Jeshi la Korea Kaskazini limefanya gwaride kubwa, kuadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwa chama tawala cha wafanyakazi. Gwaride hilo lilifanywa mapema katika uwanja wa Kim Sung wa pili kwenye mji mkuu wa Pyongyang. Maandalizi ya gwaride hilo yamekuwa yakishuhudiwa kwa wiki kadhaa za hivi karibuni.
Aidha, tangu kusambaratika kwa mkutano wa kilele na Rais wa Marekani, Donald Trump Februari mwaka 2019, mazungumzo ya kutaka kudhibiti silaha za nyuklia nchini Korea Kaskazini nayo pia yamekwama kwa sasa.
Pia Kim Jong Un aliapa mwishoni mwa mwaka 2019 kuwa Taifa lake lipo imara na linajiandaa kwa mkakati mpya wa silaha za nyuklia.
“Kama nguvu yoyote ikitumika kwa ajili ya kulishambulia taifa letu, nasi tutatumia nguvu ya kipekee kutoa adhabu ya kutosha kwa mtu au taifa husika,"amekaririwa Kim katika hotuba ya leo.