Serikali ya Tanzania ndani ya kipindi kifupi kijacho inatarajia kutoa leseni zingine mbili za uchimbaji mkubwa wa madini,anaripoti Asteria Muhozya na Tito Mselem Singida (WM) Singida.
Leseni hizo zinakuja ikiwa ni baada ya kuzinduliwa kwa ujenzi wa mgodi mpya wa uchimbaji dhahabu wa kati wa Singida Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining Company Limited. Tayari Shanta ina miliki mgodi mwingine wa kati wilayani Chunya wa New Luika.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wa pili kutoka kushoto akiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali wakielekea kwenye uzinduzi wa ujenzi wa mgodi mpya wa Shanta Gold uliofanyika Oktoba 16, 2020 mkoani Singida.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakati akizindua ujenzi wa mgodi mpya wa kati wa Singida Gold Mine Oktoba 16,2020 wilayani Ikungi mkoani Singida baada ya ujenzi wake kusubiriwa kwa muda wa miaka nane.
“Baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini watu wasio na nia njema na nchi yetu walisema mabadiliko yatawafanya wawekezaji wakimbie. Nataka niseme siku si nyingi tutatoa leseni zingine mbili (2) za uchimbaji mkubwa,”amesisitiza Naibu Waziri.
Kufutia uwekezaji huo, Naibu Waziri Nyongo ameitaka Shanta kutoa kipaumbele kwa wananchi wa Ikungi na Singida kwa ujumla katika ajira na manunuzi ya bidhaa mbalimbali. Aidha, amewaasa wachimbaji wadogo kushirikiana na mgodi ili kuweza kunufaika na uwepo wa migodi huo na si kuwa chazo cha kukwamisha maendeleo ya mgodi.
“Nimesikia Mwakilishi wa shanta akisema imelipa shilingi bilioni 3 za fidia kwa wananchi na waliopisha shughuli za mgodi na ujenzi na makazi mapya. Nawapongeza sana kwa kufanikisha hilo,’’amesema Naibu Waziri Nyongo.
Vilevile, Naibu Waziri Nyongo ametumia fursa hiyo kuikumbusha migodi yote mikubwa na ya kati inayofanya shughuli zake nchini kuanza kutoa gawio kwa Serikali ili kufuata mfano wa Twiga Minerals na kuongeza kuwa, gawio hilo linapaswa kutopungua asilimia 16 kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
Ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika Sekta ya Madini na kurejea kauli iliyotolewa hivi karibuni na Rais Dkt.John Magufuli aliyesisitiza taasisi zinazohusika kuhakikisha zinaweka mazingira rafiki ya uwekezaji huku akitaka pande zote mbili yaani Serikali na wawekezaji kunufaika sawa kwa kile alichokiita utaratibu wa Win-Win situation.
Akizungumzia mafanikio ambayo yamepatikana baada ya mabadiliko yaliyofanywa kwenye sekta ya madini ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sekta, Nyongo amesema mapato ya Serikali yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka wa fedha 2014/15 hadi bilioni 528 mwaka wa fedha 2019/20.
“Tulifanikiwa kuvuka Lengo la Mwaka 2019/20 zilizopangwa na Serikali na kuweza kukusanywa Shilingi Bilioni 528 sawa na asilimia 112.4,”amesema Naibu Waziri Nyongo.
Akizungumzia mipango ya wizara kwa mwaka 2020/2021 amesema, wizara imepangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 526.9 na kuongeza kuwa, kutokana na namna mwenendo wa makusanyo unavyoendelea anaamini kufikiwa kwa lengo kwani kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba, 2020 tayari zimekusanywa shilingi bilioni 165.29 sawa na asilimia 126.
Ameongeza kwamba, ndani ya kipindi cha miaka Mitano ya Rais Magufuli, yamekuwepo mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo Masoko 37 na Vituo 38 vya Ununuzi wa Madini vimefunguliwa na hivyo kuongeza mchango wa sekta.
“Rais Dkt. Magufuli ana maono kwamba Sekta ya Madini itachangia asilimia 10 ifikapo Mwaka 2025. Hii itawezekana tu kama tutaendelea kuanzisha Migodi mikubwa, ya Kati na Midogo. Lazima tufanye kazi na wawekezaji kwa Mujibu wa Sheria zilizopo,’’amesisitiza Naibu Waziri.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Kampuni ya Shanta Philbert Rweyemamu amesema, ujenzi wa mgodi huo unatarajiwa kutumia miezi 24 ya ujenzi wake na uzalishaji utaanza Robo ya Nne ya Mwaka 2022. Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akikata utepe kuzindua ujenzi wa mgodi mpya wa Shanta Gold uliofanyika tarehe 16 Oktoba, 2020 mkoani Singida
"Inabidi tumshukuru Mungu. Tuliisubiri siku hii kwa miaka minane sasa tangu Serikali itoe leseni tatu za Uchimbaji kwa SHANTA MINING COMPANY LTD,’’amesema Rweymamu.
Ameeleza kuwa, hadi sasa kampuni ya SHANTA imewekeza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 25 sawa na Bilioni 57 za Kitanzania katika kuiendeleza leseni zake kupitia utafiti, ajira, vibali, ulinzi pamoja na shughuli za maendeleo ya jamii.
Akieleza uwezo wa mgodi huo kuzalisha amesema kuna mashapo saba (7) yenye uwezo wa kuzalisha wakia 243,000 sawa na kilo 7,500 za Dhahabu katika miaka minane ya mwanzo wa uhai wa mgodi huo.
Amebainisha kuwa, tathmini ya kiuchumi inaonesha katika uzalishaji wa wakia 32,000 sawa na kilo 1,000 za dhahabu kila mwaka katika miaka 7 ya mwanzo kwa bei ya Dola za Marekani 1,700 kila wakia, mtaji unaohitajika kujenga mgodi wa Dola Milioni 40 za Kinarekani zitarudishwa baada ya miaka mitatu ya kwanza ya uzalishaji.
‘’Uhakika wa uzalishaji wetu upo katika kina cha mita 120 ikiwa na maana ya kuwa bado mashapo yanaendelea kwa kina. Mgodi huu utakapoanza uzalishaji utaipandisha SHANTA kufikia uzalishaji wa zaidi ya wakia Laki na ishirini (120,000) kwa Mwaka sawa na kilo 3,800 za Dhahabu,"amesema Rweyemamu.
Rweyemamu amefafanua kuwa, mgodi huo mpya unategemea katika miaka minane ya kwanza ya uzalishaji, kampuni itachangia Dola za Kimarekani Milioni 82 sawa na Bilioni 190 za Kitanzania ikiwa ni kodi na tozo mbalimbali.
Akielezea kuhusu chanzo cha kuanzishwa mgodi huo amesema SHANTA iliamua kuanza ujenzi wa mgodi kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ambavyo ni uzalishaji kutoka mgodi wake wa New Luika Gold Mine uliopo wilayani Chunya.
‘’Kampuni ya SHANTA inatoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. John Magufuli kwa maono yake ya kutumia Madini yapatikanayo Nchini kwa Maendeleo ya Taifa zima,’’ameongeza.
Akizungumzia kuhusu kulipa kodi za Serikali amesema, kampuni hiyo inaheshimu na kuzingatia sheria mpya ya madini inayoipa Serikali kwa niaba ya wananchi, umiliki wa asilimi 16 pamoja na maelekezo yake na hivyo, inatarajia kulipa hizo.
Akizungumzia ajira amesema, mgodi unatarajia kuajiri watu mia mbili (200) na manunuzi mengi pamoja na ajira zitatokea katika Wilaya ya Ikungi na kuongeza,” kampuni ya ya SHANTA imeajiri wafanyakazi zaidi ya Mia Saba ( 700) kwa Sasa na wataongezeka na kufikia Mia Tisa (900)’’. Mkuu wa Mkoa wa Singida Rehema Nchimbi akizungumza jambo kwenye uzinduzi wa ujenzi wa mgodi mpya wa Shanta Gold uliofanyika tarehe 16 Oktoba, 2020 mkoani Singida.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi ametaka uwepo wa mgodi huo wa Singida Gold Mine ambao ni mkubwa ni lazima uufanye Mkoa wa Singida usimame katika thamani yake huku ukitambulisha sifa na thamani ya Singida kutoka kwenye historia ya ukame, njaa na umaskini.
‘’Tunataka Singida itoe gawio kwa Serikali ambayo itakabidhiwa na SHANTA. Tunaamini chini ya ulezi na Usimamizi wa Wizara tutaweza,’’amesema Dkt.Nchimbi.
Akitolea mfano wa Geita kwa namna ulivyonufaika na uchumi wa madini, Naibu Waziri wa Maliasili Costantine Kanyasu amewataka wananchi wa Singida kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia mgodi huo badala ya kuilalamikia kampuni hiyo. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu akizungumza jambo kwenye uzinduzi wa ujenzi wa mgodi mpya wa Shanta Gold uliofanyika tarehe 16 Oktoba, 2020 mkoani Singida.
‘’Kwetu Geita, madini yamebadilisha maisha na kuleta maendeleo kwa mkoa. Tumetenga shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya mikopo kwa vijana na kina mama ili kubadilisha maisha ya watu. Maendeleo mkoani Geita yametokana na mapinduzi makubwa ya kisekta yaliyofanywa na Serikali,’ameelezea Kanyasu.
Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina amesema, “hata sisi wachimbaji Wadogo tutafungua Migodi mikubwa na tutatengeneza matajiri na tayari tumeanza Mirerani,’’.
Aidha, alitoa shukurani kwa Kampuni ya Shanta kwa kuahidi kutoa mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo.