Katibu Mkuu CCM Taifa asema wamejipanga vema, ateta na wazee Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Bashiru Ally amesema kuwa, chama hicho kimejipanga vyema katika uchaguzi mkuu na hakuna atakayetumia fedha zake kununua wapiga kura, kwani ni mwiko kwa mwana CCM kutumia fedha kurubuni wapiga kura.
Dkt.Bashiru ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2020 katika mkutano wake na Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinzuzi (CCM) Zanzibar.
Mkutano uliofanyika katika Ofisi Kuu za chama hicho Kisiwandui, Unguja jijini Zanzibar ambapo amesema, kampeni za CCM zinaendeshwa kwa misingi minne ambayo ni kujitegemea, nidhamu, ajenda ya uchaguzi na kuwa na wagombea wanaoweza kuanza na kufika mwisho wa uchaguzi. “Chama kina nguvu ya kuunganisha Watanzania ndiyo dhambi yetu, tuna viongozi wenye msimamo wa kulinda rasilimiali za nchi hii ndiyo dhambi yetu, tumeapa kuulinda Muungano wa Serikali mbili kwa gharama yoyote ndiyo dhambi yetu.
“Ukiona mtu anatafuta kura na anatembeza bakuli za pesa, unajiuliza anaomba kura au anaomba pesa? Ujue huyo hajajiandaa, kwa sababu Uchaguzi ulijulikana tangu 2015,”amesema Dkt.Bashiru.
Pia amesema, chama kinathamini na kuzienzi juhudi za wazee, kwani
walitumia nguvu zao katika chama wakati wa ujana wao hivyo chama
kitaendelea kuwatunza wazee hao.
“Yote ninayoyasema kuhusu
maslahi ya wazee, maisha ya wazee, makazi ya wazee, huduma kwa wazee
yameainishwa katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),"amesema.