"Ninawaomba mniletee wabunge na madiwani wa CCM ili kulisukuma jiji hili katika mpango mpya, bado nina moto mkali na Dar es Salaam, mwili wangu unawashawasha kwa ajili ya kuliletea jiji hili maendeleo, katika huduma za afya tumepanga kufanya mabadiliko makubwa sana, kwani Dar es Salaam ina watu milioni sita ni karibu mikoa mitatu au minne ambapo mwaka 2030 jiji hili linakadiriwa kuwa watu milioni 10 ndio maana mipango yake inatakiwa ifanywe leo;
Dkt.Jonh Pombe Joseph Magufuli ambaye ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameyasema hayo leo Oktoba 9,2020 wakati akiwahutubia maelfu ya wanachi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.Mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameyasema hayo wakati akiwaomba wananchi wa Dar es Salaam kura ifikapo Oktoba 28,mwaka huu kwa nafasi ya urais, ubunge na madiwani wote wa CCM.
Amesema, miaka mitano ijayo anatarajia kufanya Dar es Salaam kuwa jiji la mfano barani Afrika kwa kuhakikisha anaimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara za juu, chini,upanuzi wa bandari pamoja na ukamilishaji wa mradi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Rais Magufuli mesema, anataka watu watakapofika jijini Dar es Salaam wajue sio Afrika bali wajue wapo Ulaya kutokana na maendeleo yatakayofanyika ndani ya kipindi hicho cha miaka ijayo katika jiji hilo la kibiashara.
Amesema, wananchi wa Dar es Salaam wana uamuzi wa kuamua kuwa na maendeleo kwa kumchagua yeye au kutokuwa na maendeleo kwa kuwachagua watu wengine. Dkt.Magufuli amesema, mwaka 2015 alipoingia madarakani aliwaambia ataibadilisha Dar es Salaam, "tutajenga flyover hakuna mtu aliyeamini,lakini leo hii mnajionea wenyewe,”amesema Dkt.Magufuli.
Rais Magufuli amesema,miaka mitano ijayo wamejipanga kuimarisha miundombinu ya usafiri ,kukamilisha miradi ambayo haijakamilika ni pamoja na mradi wa barabara ya Moroco,Mwenge, Bamaga Shekilango, Kimara, Kibaha barabara ya Pungu,Kifuru,Mbezi Mwisho hadi Mpiji Magoe.
Amesema, wanatarajia kukamilisha mradi wa pili wa mabasi ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Mbagala, daraja la Salendar na daraja la juu la gerezani pia kukamilisha miradi ya kimkakati ya upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa reli ya Dar es Salaam hadi Dodoma.
Magufuli amesema, sambamba na hayo wamepanga kufanya upanuzi wa barabara ya bandari, TAZARA, uwanja wa ndege, Morocco, hadi Kawe, Makongo, Mbagala Kongowe na kuaanza ujenzi wa awamu ya tatu ya mabasi ya mwendokasi kutoka Barabara ya Nyerere, Bibi titi hadi Azikiwe na huku awamu ya nne ikiendelea na Barabara ya Maktaba Nyerere, Ali hassan Mwinyi, Samnujoma hadi Tegeta
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Dkt.Bashitu Ally amesema wanapoelekea mwishoni mwa kampeni wanafanya kampeni kwa mtindo wa bandika bandua na wamekubaliana katika kuzingatia yale ambayo waliyoelekezwa na mgombea urais wa CCM,Dkt.John Magufuli ya kuhakikisha wanafuata misingi ya uhuru wa Taifa kutolegeza wala kulegezwa na mtu yeyote ndani na nje.
Amesema, kwa sasa CCM wamezindua awamu ya tano ya kampeni ambapo mgombea urais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atazunguka katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam.
“Tangu Oktoba 2, mwaka huu Dkt.Magufuli ameingia Dar es Salaam amefanya kazi za kitaifa na leo anaanza tena kufanya kampeni kwa awamu ya tano hapa.Sekretarieti ilieleza ikupangie mikutano minne hapa, leo ni mkutano wa kwanza ambapo tumepanga kuwafikia wapiga kura wa majimbo matatu Kigamboni,Temeke na Mbagala,”amesema.
Amesema, mkutano wa pili utakuwa Kinyerezi kwa majimbo ya Segerea,Ilala na Ukonga huku mkutano wa tatu unatarajia kuwa katika uwanja wa Barafu Mburahati utahusisha majimbo ya Ubungo na Kibamba na mkutano wanne utakuwa katika uwanja wa Tanganyika Peckars kwa majimbo ya Kawe na Kinondoni jijini humo.
Amesema, kufanyika kwa mikutano hiyo ni kutokana na ukubwa wa jiji hilo na kuweza kuwafikia wapiga kura wengi kwa wakati mmoja.