Taifa Stars wakicheza pungufu kwa 12' wamechapwa bao 1-0 na Burundi ‘Int’hamba Murugaba katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa katika Jiji la biashara Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika mchezo wa leo Oktoba 11,2020 ambao mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kipindi cha kwanza timu zote mbili zilitoshana nguvu baada ya kwenda vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa hawajafungana bao lolote.
Aidha, kipindi cha pili mambo yalizidi kuwa magumu kwa timu zote mbili ambapo Taifa Stars ilijaribu kufanya mashambulizi, lakini yalishindwa kuzaa matunda na Burundi ilikuwa ya kwanza kupiga shuti la kwanza ambalo lililenga lango kipindi cha pili.
Jonas Mkude alitolewa kwa kadi nyekundu 78' baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumvaa na kumkunja Saidi Ntibazonkiza baada ya wawili hao kuchezeana rafu wakati wa mtanange huo.
Aidha,kiungo huyo wa FK Kaisar Kyzylorda ya Kazakhstan, Ntibazonkiza ndiye aliyeifungia Burundi bao hilo pekee 86' akimalizia pasi ya mkongwe Cedric Amissi wa Al Taawon ya Saudi Arabia katika mchezo huo wa kirafiki.