Matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kwenye upande wa Wagombea Urais yameanza kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Oktoba 29, 2020, katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, anaripoti LILIAN SHEMBILU (MAELEZO).
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Joseph Pombe Magufuli anaongozakwa wingi wa kura kwenye matokeo ya awali ya majimbo 76 huku akipata asilimia 98.72 katika Mkoa wa Mwanza Jimbo la Misungwi, huku akiwaacha mbali wagombea wengine.
Matokeo hayo yanaendelea kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji (Mst) Semistocles Kaijage, amesema watakuwa wanatangaza kwa awamu kutokana na jinsi watakavyoendelea kupokea matokeo hayo kutoka kwenye majimbo mbalimbali nchini.
Majimbo ambayo yamekwisha kutangazwa ni pamoja na Njombe Mjini, Mkoa wa Katavi Jimbo la Nsimbo, Misungwi na mengineyo ambako Mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dkt John Pombe Magufuli anaongoza kwa wingi wa kura akifuatiwa na Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu.
Katika Majimbo hayo Dkt.Magufuli ametia fora katika majimbo ya Misungwi alikojizolea kura nyingi na kupata asilimia 98 na Jimbo la Nsimbo akipata kwa asilimia 95 na kuwazidi wapinzani wake wa vyama vingine vilivyoshiriki katika kinyang’anyiro cha nafasi ya urais.