MAJALIWA: TANZANIA INAHITAJI KIONGOZI MADHUBUTI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema suala la kuchagua kiongozi wa kuliongoza Taifa ni muhimu na halihitaji ushabiki, hivyo amewataka wananchi wahakikishe ifikapo siku ya kupiga kura wakachague kiongozi madhubuti atakayewaletea maendeleo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kikunde wilayani Kilindi wakati alipowaomba wampigie kura Mgombe Urais wa CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mbunge na Madiwani wa CCM, Oktoba 8, 2020. (Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Tunatafuta viongozi wa kuliongoza Taifa ambao ni Rais, wabunge na madiwani, nawaomba ifikapo Oktoba 28 mwaka huu tujitokeze kwa wingi kwenda kumchagua mgombea wa urais wa tiketi ya CCM Dkt. John Pombe Magufuli kwani ni kiongozi pekee atakayeweza kuwaongoza wananchi wote bila ya kujali itikadi zao vyama vyao.”

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 8, 2020 alipozungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Kata za Kikunde, Tunguli na Kwekivu wilayani Kilindi, Mkoa wa Tanga katika mikutano ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Kilindi Omari Kigua na wagombea wa udiwani wa CCM.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi ambaye ameingia katika nafasi hiyo si kwa majaribio bali ni mtu ambaye anajua na anauwezo wa kuwatumikia wananchi na mfano ameuonesha katika kipindi cha miaka mitano ya awali ambayo ameongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.

“…Ombi hili ni kwa Watanzania wote haliangalii wewe ni wa chama gani, halina ushabiki nawaomba wote tukamchague Dkt. Magufuli kwa nafasi ya urais, wabunge na madiwani wa CCM nchini kote ili waweze kushirikiana kuwaletea maendeleo. Nawaomba muendelee kuwa na imani na Serikali ya CCM kwani imedhamiria kuwatumikia.”

Amesema ni muhimu wananchi wote wahakikishe wanawachagua viongozi wanaotokana na CCM kwa sababu ni chama chenye ilani inayotekelezeka tofauti na vyama vingine. “CCM ndio jiko linaloweza kupika maendeleo, tukampigie tena kura Dkt. Magufuli kwa sababu mnamjua na mmesikia na kuona maendeleo aliyoyaleta nchini.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wananchi hao kwamba vijiji vyote katika wilaya hiyo ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme vitafikiwa. Wilaya hiyo ina vijiji 102 kati yake vijiji 52 tayari vimeshaunganishiwa umeme na vilivyosalia 50 tu navyo vitaunganishiwa.

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Kilindi. Gharama za kuunganishiwa umeme huo amezipunguza kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 tu.

 Pia Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala hawatalipia fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news