Majaliwa:Jiandaeni kutumia fursa ya reli ya kisasa na Bandari kavu

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewakata wakazi wa Isaka, wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wawe tayari kutumia fursa ya ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa bandari kavu ili kujiletea maendeleo.

Ametoa wito huo leo Oktoba 2, 2020 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Kagongwa na Isaka akiwa njiani kuelekea kata ya Kakole katika jimbo la Msalala.

Amesema Isaka ni kitovu kikubwa cha biashara kwa sababu kuna miradi mikubwa miwili ambayo itatekelezwa. “Kwanza kutakuwa na bandari kavu ambayo itakuwa inapokea mizigo kutoka nchi tofauti zinazotuzunguka. Kwa hiyo wana Kagongwa, tumieni fursa hii kufanya biashara. Wana Isaka tumieni fursa hii kujenga nyumba za kulala wageni na mahoteli ya kuuza vyakula.”

“Pili ni reli ya kisasa ambayo tunapanga kuijenga itapita hapa Isaka. Reli hii ikikamilika, mtu atakuwa anatumia saa nne kwenda Dar es Salaam badala ya saa 14 ambazo zinatumika hivi sasa kwa usafiri wa mabasi.”

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Shinyanga kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea udiwani wa jimbo la Msalala. Mgombea ubunge wa jimbo la Msalala, Bw. Iddi Kassim Iddi amepita bila kupingwa.

Wakati huohuo, akizungumza na wakazi wa Kata za Segese na Kakola, Mheshimiwa Majaliwa amesema barabara ya kutoka Geita kupitia Kagongo hadi Kahama yenye urefu wa km. 106 itajengwa kwa kiwango cha lami.

"Barabara hii ilikuwemo kwenye ilani inayomalizika sasa uk.66 na ilipangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu lakini katika ilani yetu ya sasa, inatakiwa kukamilishwa ili wananchi muanze kufanya biashara kwa urahisi."

Katika hatua nyingine, akimuombea kura Rais Magufuli kwenye mikutano huo, mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Bw. Patrobas Katambi amesema wakazi hao wana kila sababu ya kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa vile kina sera za kuwaendeleza watu wa makundi tofauti wakiwemo vijana na wanawake.

"Ndugu zangu msidanganywe, tarehe 28 twendeni tukamchangue Dkt. Magufuli, mbunge na madiwani wa CCM kwa sababu watatuletea maendeleo. Usipoteze muda, kwa mjomba hakuna urithi. Rudi nyumbani kumenoga," amesema.

Aliwataka wakazi hao wajihadhari wasiwachague wagombea wa upinzani kwani wameahidi kuweka rehani madini ya Tanzania ili wapate fedha endapo watachaguliwa kuongoza nchi. "Wamesema wataweka madini yetu rehani ili wapate fedha, sasa tukiwapa nchi, si watatuweka na sisi rehani?" Alihoji.

Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na ziara ya kumuombea kura Dkt. Magufuli katika jimbo la Kahama Mjini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news