Serikali ya Marekani imeueleza mkutano wa Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO) kwamba haimuungi mkono raia wa Nigeria, Ngozi Okonjo Iweala kuongoza shirika hilo.
Kwa mujibu wa Reuters, hayo yanajiri licha ya Okonjo kupata uungwaji mkono kutoka mataifa yaliyo nje ya bara la Afrika.
Imeelezwa kuwa,msimamo huo wa Marekani unaweza kuidhoofisha taasisi hiyo ya biashara duniani ambayo inaendelea na mchakato wa kumpata kiongozi atakayechukua nafasi ya Mkurungezi wa WTO raia wa Brazil Roberto Azevedo ambaye alijiuzulu mwezi Agosti, mwaka huu.Awali, kundi kubwa la mabalozi wa WTO walipendekeza Okonjo Iweala awe mkurungezi wa shirika hilo, lakini uamuzi huo unahitaji makubaliano kati ya nchi 164 wanachama wa WTO, ikimaanisha kwamba nchi yoyote inaweza kuzuia uteuzi wa Okonjo kushika wadhifa huo.