Mbinga yatengeneza hatimiliki za kimila zaidi ya 26,000

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amezindua mpango wa kugawa hati miliki za kimila zaidi ya 1000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mndeme amezindua hatimiliki hizo katika Kijiji cha Nyoni kati ya hatimiliki zaidi ya 26,000 zilizotengenezwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya kugawawiwa vijiji 86.

Mndeme amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ametimiza ahadi aliyotoa kwa watanzania ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika kwa kupanga kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi kwa kila mwananchi.

Mndeme amevitaja vijiji vitano vya Kata ya Nyoni ni kati ya vijiji 86 ambavyo vimenufaika na mpango wa hati miliki za kimila katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akimkabidhi mmoja wa wananchi hatimiliki katika Kata ya Nyoni Mbinga.
Katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewakabidhi hati wakulima 20 wa Kata ya Nyoni kwa niaba ya kata 24 zilizopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

“Naomba kuanzia sasa watu wa benki mzitambue nyaraka hizi za hati miliki za kimila kuwa ni halali na wanaweza kuzitumia sehemu yeyote na vyombo vya kisheria kwa sababu mashamba haya yanakwenda kutambulika rasmi,”amesema Mndeme.

Mndeme pia amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kufanikisha zoezi hilo ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja katika upimaji wa mashamba ambao umehusisha vijiji 86 vyenye ekari takribani 59,000.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akikata utepe kuashiria uzinduzi wa hati za kimila Hlalmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye amesema atahakikisha kila kipande ambacho kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kinapimwa ambapo ametoa rai kwa wananchi ambao hawajapimiwa kuondoa hofu kuhusu zoezi hilo ambalo ni endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele, amesema ekari 70,000 ya mashamba ya mazao ya kudumu ambayo ni sawa na mashamba 26,247 yametambuliwa na kupimwa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipozindua mpango wa ugawaji wa hatimiliki za kimila Kata ya Nyoni Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Hata hivyo Mnwele amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeweza kutengeneza hatimiliki za kimila 26,247 katika vijiji 86 zilizogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na vijiji hivyo ni kati ya vijiji 117 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Naye mkulima wa kijiji cha Nyoni, Ponziana Nzuyu amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kuwaunga mkono wakulima ambapo ametoa rai kwa wataalam kuendelea kuwaelimisha wananchi faida za hatimiliki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news