Miundombinu bora ni kielelezo cha kuyaenzi Mapinduzi Matukufu asema Rais Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amesema kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya miundombinu ni kielelezo cha kuyaendeleza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwa shabaha ile ile ya kuwakomboa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo ya uhakika.
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein (katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya Ufunguzi wa Barabara ya Kombeni-Fuoni iliyojengwa na Kampuni ya "CHINA CIVIL ENGINEERING CORPRATION"(CCECC) kutoka China ambapo Serikali imegharamia ujenzi huo, hafla iliyofanyika Kombeni Wilaya ya Magharibi "B" Mkoa wa Mjini Magharibi,Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (katikati) Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi (wa pili kulia) na Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji, Dkt.Sira Ubwa Mamboya. (IKULU).
Dkt.Shein ameyasema hayo Oktoba 2,2020 huko Kombeni wakati akiwahutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Kombeni hadi Fuoni iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa barabara ya Koani hadi Jumbi.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Mapinduzi ndiyo yaliyokomboa kila kitu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwani kila kitu cha maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba kilianza mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Akieleza historia ya miundombinu ya barabara Zanzibar, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Idara ya Kazi ya Barabara (PWD) ndio iliyokuwa ikifanya kazi ya barabara mpya pamoja na zile za zamani mara baada ya Mapinduzi na baadae ikabadilika na kuitwa Idara ya Ujenzi na Utengenezaji wa Barabara (UUB).

Rais Dkt.Shein amesema kuwa, hatua ya ujenzi wa barabara hizo pia ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 na kutumia fusra hiyo kuipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasilino na Usafirishaji kwa kusaidia katika utekelezaji wa ilani hiyo.

Amesema kuwa, shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinategemea miundombinu ya barabara zilizo bora ambapo pia, juhudi za kuimarisha kilimo,utalii,uwezeshaji na sekta zote za kiuchumi kunahitaji kuwepo kwa barabara za kisasa.

Ameongeza kuwa, kuimarika kwa miundombinu ya barabara ndio chachu ya maendeleo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kwa kasi sana kuimarisha miundombinu ya barabara ili itoe msukumo katika jitihada za kuendeleza sekta nyingine.

Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kuendelea kuitekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kusimamia ahadi alizozitoa katika nyakati mbali mbali za uongozi wake huku akiipongeza Kampuni ya “China Civil Engineering Construction Corporation” (CCECC).

“Nimefarajika kuona kwamba tumefanikisha kumalizika kwa barabara hizi tatu nilizoahidi kuzimaliza kabla ya muda wangu wa uongozi kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kumalizika ambazo ni Fuoni-Kombeni, Koani-Jumbi kwa Unguja na Ole-Kengeja kwa Pemba,"amesema Dkt.Shein.

Rais Dkt.Shein alitumia fursa hiyo kwa kusema kuwa ujenzi wa barabara ya Ole-Kengeja nao umeshamaliza na imani yake atakapokwenda Pemba wiki ijayo ataizindua ambayo ina urefu wa kilomita 35 huku akieleza kuwa kipande cha barabara cha kutoka Bububu hadi kwa Nyanya nacho tayari kimeshakamilika.

Aidha, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, faida zinazopatikana katika uendelezeji wa miundombinu ya barabara zinatokana na uamuzi uliochukuliwa na Serikali wa kununua vifaa vipya vya ujenzi wa barabara vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni 14.

Rais Dkt.Shein pia, alitumia fursa hiyo kuihimiza Wakala wa Barabara kuwa na mipango imara ya kuzifanyia ukarabati barabara huku akiwataka wafanyakazi wa Wakala wa Barabara kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kwa kwenda na wakati uliopo kwani tayari Serikali imo katika mchakato wa kuwaongezea mishahara ili walipwe vizuri.

Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara mpya katika maeneo yanayohitajika ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia matengenezo barabara za ndani ya miji kwa kuzipanua na kujenga barabara mpya ambapo mipango hiyo ni muhimu katika juhudi za kupambana na tatizo la msongamano wa gari ndani ya miji.

Nae Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dkt. Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa uzinduzi wa barabara hizo ni mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt.Shein.

Alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein wa Awamu ya Saba ambapo zaidi ya kilomita 300 za barabara zimejengwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa ujenzi wa barabara hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji mjini na vijijini kwa lengo la kuwaondoshea wananchi shida ya usafiri ambapo Wizara yake imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara Unguja na Pemba.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Kombeni hadi Fuoni yenye urefu wa kilomita 8.5 na Koani Jumbi kilomita 6.3 iliyopo Wilaya ya Kati Unguja.

Alisema kuwa hizo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kujenga ustawi wa wananchi wake kwa kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya barabara za mjini na vijijini Unguja na Pemba.

Aidha, alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kama ilivyoelezwa kwenye ukurasa wa 138 kifungu cha 83, kifungu kidogo cha b na c, Dira ya Maendeleo (Vision 2020), MKUZA III, Sera ya Taifa ya Usafiri pamoja na Mpango Mkuu wa Usafiri Zanzibar.

Mradi wa ujenzi wa barabara hio ya Kombeni hadi Fuoni yenye urefu wa kilomita 8.5 ni miongoni mwa barabara nne ikiwemo ile ya Bububu, Chuini kuelekea Mahonda hadi Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 31, Pale-Kiongele yenye kilomita 4.61, Matemwe-Muyuni Kilomita 7.58 Bububu Polisi hadi Chuini yenye urefu wa kilomita 2.8.

Aliongeza kuwa barabara zote hizo zimekamilika kwa kiwango cha lami na kazi zinazoendelea ni ujenzi wa misingi ya maji ya mvua pembezoni mwa barabara pamoja na kuweka alama za usalama za barabarani pamoja na kujengwa kwa vizuizi kwenye baadhi ya sehemu ya miinuko..

Alisema kuwa ujenzi wa barabara hizo umetekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Fuoni hadi Kombeni ulianza tarehe 17 Agosti 2019 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 30 mwezi Septemba mwaka huu ambapo mradi huo ulitiliana saini tarehe 8 Novemba mwaka 2017 baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji na Mjenzi ambaye ni Kampuni ya ‘China Civil Engineering Construction Corporation’ (CCECC), kwa thamani ya TZS Bilioni 71.9 kwa barabara zote 4 ambapo kwa barabara ya Fuoni – Kombeni iligharimu TZS Bilioni 9.1 na mchango wa SMZ ulikuwa ni TZS Bilioni 3.120.

Aliongeza kuwa Msimamizi wa Mradi ni Kampuni ya H.P Gauff Ingenieure GmbH ya Ujerumani ambae alifungiana Mkataba na Wizara hiyo tarehe 15 Julai 2017 kwa thamani ya Euro Milioni 1.5. ikiwa ni sehemu ya mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.

Kwa upande wa barabara ya Jumbi hadi Koani yenye urefu wa kilomita 6.3 Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ujenzi huo umegharamiwa kwa pamoja kati ya SMZ pamoja na mkopo wa Benki ya BADEA kwa gharama ya TZS bilioni 5. 690 ambapo SMZ imechangia TZS bilioni 1.95 ambapo kazi ya ujenzi imefanywa na Kampuni ya MECCO ya Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Wakala wa Barabara huku akisema kuwa barabara ya Kizimbani hadi kiboje matayarisho yake tayari yameanza.

Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia (CCM) Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kusaidia kuruhusu kujenga barabara hiyo iliyopita sehemu ya Jeshi bila ya fidia na malipo yoyote pamoja na kutoa shukurani kwa uongozi na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo.

Viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeid Ali Maulid, Mawaziri na viongozi mbali mbali wa Serikali pamoja na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi wa maeneo zilimopita barabara hizo.

Rais Dk. Shein akiwa ameambatana na viongozi pamoja na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo walipata fursa ya kuzitembelea barabara hizo zote mbili ambapo pia, aliifungua kwa kuweka jiwe la msingi na kukata utepe barabara ya Jumbi hadi Koani hapo katika eneo la Jumbi bango la Mkoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news