Mkutano wa mafanikio ya miaka 20 na matarajio ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefanyika jana kwa njia ya video katika nchi nne za China, Afrika Kusini, Botswana na Nigeria.
Washiriki wa mkutano huo wamejadili kuhusu mafanikio yaliyopatikana na baraza hilo katika miaka 20 iliyopita, hali ya sasa na mwelekeo wa maendeleo kati ya China na Afrika, pamoja na mfumo wa maendeleo kati ya pande hizo.
Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Lugha za Kigeni ya China, Lu Cairong akihutubia mkutano huo ameeleza kuwa, kutokana na baraza hilo, maeneo ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili na nguvu ya ushirikiano vimeongezeka.
Mwenyekiti wa Kamati za Bunge la Afrika Kusini, Cedric Frolick amesema, sababu kubwa ya kuhimiza maendeleo ya kasi ya uhusiano kati ya pande hizo mbili ni pamoja na urafiki mkubwa na wa kudumu kati ya China na nchi za Afrika, ushirikiano wa kiuchumi wenye usawa na kunufaishana, pamoja na kuaminiana katika mambo ya kisiasa.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Mambo ya China cha Nigeria, Charles Onunaiju amesema, Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika kwa kushirikiana na Pendekezo la "Ukanda mmoja, Njia Moja" linachangia katika kuhimiza mafungamano barani Afrika.