Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Tanzania, Burundi na Rwanda) katika Mto Kagera, umetajwa kuwa ni kielelezo bayana kinachoonesha uimara wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya siku nne ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya mtangamano inayounganisha nchi wanachama wa EAC, iliyofanyika katika mikoa ya Kigoma na Kagera kuanzia tarehe 28 hadi Oktoba Mosi, 2020.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote pamoja na ujumbe wao wakitemba kwa miguu kuelekea katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani cha Rusumo. (Mambo ya Nje).
Katika ziara hiyo, Balozi Ibuge alifanikiwa kutembelea ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 310 kutoka Nyakanazi-Kasulu hadi Manyovu, Mpaka na Burundi; Barabara ya kikanda (Tanzania/Uganda ya Bugene-Kasulo-Kumunazi (133 km); Kyaka-Mutukula (30 km)/Mutukula-Masaka (89.5 km) ambazo zinafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi; vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mpakani (OSBPs) vya Kabanga (Tanzania na Burundi), Rusumo (Tanzania na Rwanda), Mutukula (Tanzania na Uganda) ambavyo ujenzi wake umekamilika na vinafanya kazi.
Aidha, Balozi Ibuge alitembelea Eneo litakalojengwa OSBP ya Tanzania na Burundi katika Mpaka wa Manyovu/Mugina ambapo wataalam wanaendelea na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, kilichotengewa Dola za Marekani milioni 12, na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika Mto Kagera unaojulikana kama Mradi wa Kikanda wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Rusumo.
Alipokuwa Rusumo, Balozi Ibuge aliridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa umeme ambao umefikia asilimia 67 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2022. Wahandisi wa mradi huo walimweleza Balozi Ibuge kuwa ujenzi umegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha umeme (Power Plant) ambao unagharimu Dola za Marekani milioni 340.
Fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa EAC na sehemu ya pili ni ujenzi wa njia za kusafirisha umeme (Transmission lines) ambao unafanywa na mashirika ya umeme ya kila nchi. Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 128.6 kwa ajili ya ujenzi wa njia hizo na taarifa iliyotolewa ni kwamba kila nchi imeanza kutekeleza ujenzi wa njia hizo.
Wahandisi hao waliendelea kueleza kuwa mtambo huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawatti 80 ambapo kila nchi itapata mgawo wa Megawatti 27. Wahandisi walimuhakikishia Balozi Ibuge kuwa mradi huo utakamilika kwa ubora unaotarajwa, kwa kuwa wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka kila nchi mshirika.
Balozi Ibuge kwenye miradi yote hiyo aliyoitembelea, aliwasihi watumishi kutanguliza maslahi ya umma kwanza, kuliko maslahi yao binafsi.
Amesema,miradi yote hiyo inalenga kuongeza kasi ya muingiliano wa watu, biashara ya bidhaa na huduma katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo asitokee hata mtu mmoja kwa maslahi yake akajaribu kuhujumu lengo hilo la EAC.
Alihitimisha kwa kusema kuwa hivi karibuni, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alizuru Tanzania katika mkoa wa Geita na Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi alizuru nchini katika mkoa wa Kigoma. Katika mazungumzo yao na mwenyeji wao, Rais Dkt. John Pombe Magufuli walisisitiza umuhimu wa ujenzi wa miundombinu imara itakayoleta chachu ya biashara katika Jumuiya. Hivyo, aliwataka watendaji hao wasitumie dhamana waliyopewa kuwaangusha viongozi wetu.
Tags
Habari