Mwalimu Makuru Lameck Joseph awafunda wagombea Musoma Mjini asisitiza amani, upendo na mshikamano

Aliyekuwa miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitosa kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho kwenye kura za maoni kugombea Ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amewaomba wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kufanya kampeni ndani ya jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28,mwaka huu, kufuata sheria taratibu na kanuni za uchaguzi ikiwemo kutojihusisha na kutoa lugha za uchochezi zinazopelekea uvunjifu wa amani,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Mwalimu Makuru amesema, amani ndio msingi wa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla, hivyo wagombea wote na wafuasi wa vyama vyao wanapaswa kuhakikisha wanafanya kampeni za kistarabu na kujiepusha kutotumia lugha zinazohamasisha vurugu, uchochezi, ubaguzi, mgawanyiko, badala yake wafanye kampeni za kunadi sera na kusisitiza amani wakitambua kuwa baada ya Uchaguzi maisha yataendelea kama kawaida, hivyo uchaguzi usiwe chanzo cha mgawanyiko ama uvunjifu wa amani.

Ameyasema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi uliofanyika katika Kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma ambapo pia ulihudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasihi wananchi wa kata hiyo kumchagua Abas Mohamed wa Chama Cha Mapinduzi kwani ndiye aliyewafanya vijana wengi kupenda michezo na sanaa pamoja na Mbunge wa CCM na Rais Magufuli kusudi wakashirikiane kuwatumikia Watanzania kuwaletea maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

"Amani ndiyo msingi wa Taifa letu, kwa hiyo wagombea wa vyama vyote ni muhimu kuzingatia lugha zinazofaa wakati wa kampeni, amani ikitoweka wananchi hawatafanya shughuli za maendeleo, wanasiasa wasitumie majukwaa ya kampeni kuhamasisha uvunjifu wa amani, na wananchi muwe makini kutofuata lugha za uchochezi endapo watahamasisha, nchi yetu imejengwa katika misingi ya amani, umoja, mshikamano, hivyo tusiruhusu hata kidogo amani ikachezewa na pia vyombo vya usalama na mamlaka husika naomba zisisite kuwachukulia hatua watu wanao hubiri uvunjifu wa amani,"amesema Mwalimu Makuru. 

"Hakuna mtu aliyeko juu ya sheria hata kidogo, kwa hiyo Mgombea wa chama chochote akihamasisha vurugu kwa wafuasi wake nashauri mamlaka husika ichukue hatua haiwezekani kujengeana chuki sisi sote tunajenga nyumba moja kwa hiyo amani yetu katika Jimbo la Musoma Mjini na hapa nchini, lazima idumishwe kwa umoja wetu kipindi hiki cha kampeni, uchaguzi, na baada ya Uchaguzi Mkuu kufanyika,"amesema Mwalimu Makuru. 

Aliwahimiza wakazi wa Musoma Mjini kuhakikisha wanampa kura za kishindo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini ,Vedastus Mathayo pamoja na mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi,Dkt. John Pombe Magufuli kusudi akafanye kazi za kuliletea Taifa maendeleo kama ambavyo amefanya kwa miaka mitano ambapo Rais Magufuli ameliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati na kuliheshimisha kimataifa, hivyo akaomba wananchi wamchague kwa kishindo akatimize azma ya kutekeleza miradi mingine ya kiuchumi na kijamii kwa maslahi mapana ya Watanzania wote.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini,Hasan Milanga amesema kuwa, chama pekee chenye uwezo wa kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania ni CCM kwani ilani ya chama hicho imesheheni yote ambayo wananchi wanapaswa kufanyiwa, ikiwemo huduma za maji, afya, elimu, miundombinu, uchumi bora, hivyo akaomba wakichague kikatekeleze ilani hiyo kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news