NEC 'ya delete' madai ya CHADEMA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imebaini kuwepo kwa taarifa ya upotoshaji kuhusu mchakato wa zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu (2020) na jina la Mzabuni aliyeshinda zabuni hiyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 12,2020 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt.Wilson Mahera Charles mbele ya waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt.Wilson Mahera Charles akitoa taarifa ya ufafanuzi kuhusiana na madai ya upotoshaji juu ya mchakato wa za uchapishaji karatasi za kupigia kura. (DIRAMAKINI).

Dkt. Charles amesema kuwa, taarifa hiyo potofu iliyonukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii (si Diramakini) imetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw.John Mnyika wakati akizungumza na vyombo vya habari.

"Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa mujibu wa Ibara ya 74 )(6) (b)na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imepewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.

"Ili iweze kutekeleza jukumu hilo,tume imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba vifaa vya uchaguzi vinapatikana mapema, vinahifadhiwa vizuri, vinafungashwa kulingana na uhitaji na vinasafirishwa katika hali ya usalama hadi kwenye vituo vya kupigia kura,"amefafanua Dkt.Charles.

Amesema, katika kufanikisha azma hiyo, tume iliandaa mpango wa manunuzi wa vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 kwa mujibu wa Kifungu cha 49 (2) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ikisomwa kwa pamoja na kanuni kwenye GN 446 ya mwaka 2013.

"Tangazo la fursa za zabuni la ujumla (General Procurement Notice) liliwekwa kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) tarehe 2 Julai,2019 na kurudiwa tena tarehe 13 Disemba, 2019 likiwa katika mfumo wa TANePS.

"Vilevile, tume ilitangaza kwenye Gazeti la Serikali la Daily News la tarehe 8 Julai 2019 kwa ajili ya kuufahamisha umma kuhusu fursa za zabuni zitakazotangazwa baadae na tume. Umma uliofahamishwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa wakiwemo wale wa Chama cha CHADEMA,"amefafanua Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi NEC.

Dkt.Charles amesema, katika mpango huo wa manunuzi jumla ya zabuni 47 ziliorodheshwa ikiwemo zabuni Na. IE/018/2019-20/HQ/G/GE/13 iliyohusu uchapishaji wa karatasi za kupiga kura.

Dkt. Charles amesema kuwa, njia ya kumpata mshindi iliyotangazwa ni ya ushindani wa wazi wa Kimataifa (International Competetive tender), hivyo, zabuni hiyo ilitangazwa na PPRA tarehe 9 Machi, 2020 kwenye mtandao wa TANePS, ikarudiwa kutangazwa na tume kwenye Gazeti la Daily News la tarehe 10 Machi,2020. 

"Ufunguzi wa zabuni hiyo ulifanyika tarehe 8 Aprili na jumla ya makampuni yaliyoshiriki yalikuwa ni matatu yote yalitoka nje ya nchi kama ifuatavyo; M/s Ren Form CC ya Afrika Kusini, M/s Ellams Products Limited ya Kenya na M/s Al Ghurair Printing and Publishing LLC ya Dubai,"amefafanua Dkt.Charles.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news