NEC yaruhusu matumizi ya vitambulisho mbadala Oktoba 28,2020 kwa waliopoteza

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kikao chake cha Oktoba 12, 2020 imefanya maamuzi ya kisera ya kuruhusu vitambulisho mbadala kutumika kupiga kura, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yameelezwa kupitia taarifa iliyotolewa na Dkt.Cosmas Mwaisobwa kutoka Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC).

Amesema, uamuzi huo umezingatia matakwa ya Kifungu cha 61 (3) (a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 ambavyo vinaipa Tume/Mkurugenzi wa Uchaguzi mamlaka ya kuruhusu kutumika kwa utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura aliyejiandikisha kuweza kupiga kura iwapo amepoteza kadi yake ya mpiga kura ama imeharibika.

"Vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura anaruhusiwa kutumia ni kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na NIDA, Hati ya Kusafiria, Leseni ya Udereva. Hata hivyo ni sharti majina yaliyomo kwenye vitambulisho hivyo yafanane na majina yaliyomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo husika cha kupigia kura.

"Tume imefanya uamuzi huo ili kuwawezesha wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura au kadi zao zimeharibika, kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura Siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28, Oktoba,2020,"amefafanua Dkt.Cosmas Mwaisobwa kutoka Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) kupitia taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news