Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) imekabidhi kwa vyama vya siasa nakala tepe ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Sambamba
na orodha ya vituo vya kupigia kura, mfano wa karatasi ya kupigia kura
kwa nafasi ya kiti cha Rais na Makamu wa Rais na jalada la nukta nundu
(tactile ballot folder), anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi NEC, Dkt.Wilson Mahera Charles amesema, makabidhiano hayo
ya leo Oktoba 15,2020 yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 37 ya Kanuni
za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za mwaka 2018 ambayo
inaielekeza tume kuvipatia vyama vya siasa nakala ya daftari kwa ajili
ya utambuzi wa wapiga kura wanaoingia katika kituo cha kupigia kura.
Dkt.Charles
amesema kuwa, orodha ya kupigia kura imetolewa kwa vyama vya siasa ili
kuviwezesha vyama kuwasilisha orodha ya majina ya mawakala watakaopangwa
katika vituo hivyo siku ya kupiga kura.
"Vyama vya siasa
vinashauriwa kutumia mfano wa karatasi ya kura ambazo zimetolewa kwa
vyama vya siasa kuwaelimisha wanachama na wafuasi wao kupiga kura kwa
usahihi ili kupunguza idadi ya kura zinazoharibika.
"Kwa kuwa
zimebaki siku 12 kufikia tarehe 28 Oktoba, 2020 ambayo ni siku ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Tume inavitaka vyama vya siasa na
wagombea kuendelea kuzingatia maadili ya uchaguzi, kunadi sera na
kuwahimiza wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa
amani,"amefafanua Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dkt. Wilson Mahera
Charles.Video tazama hapa.