NEEMA LUGANGIRA: NITAKUWA KIUNGO MUHIMU KATI YA ASASI ZA KIRAIA NA SERIKALI

Wakati tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, wagombea wa nafasi mbalimbali wameendelea kutoa ahadi ya nini watafanya pindi watakapopata ridhaa ya wananchi kuuongoza katika nafasi wanazogombea,anaripoti Victoria Kazinja (Diramakini) Morogoro.

Neema Lugangira ni Mbunge Mteule wa Viti Maalumu (CCM) kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Tanzania Bara ambaye naye kama walivyo wengine anaahidi nini atafanya endapo atafanikiwa kuingia bungeni baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 28.

Mbunge Mteule Viti Maalum CCM Tanzania Bara, Neema Lugangira (wa pili kulia), akimsikiliza mmoja wa viongozi wa MVIWATA. (Diramakini).
“Awamu ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mengi makubwa ya maendeleo, Rais John Pombe Magufuli katika muhula wa miaka mitano ya uongozi amewekeza kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kero mbalimbali za wananchi zinatatuliwa na kwa hiyo maisha ya watu yanaboreshwa,”Anaanza kueleza Neema Lugangira alipozungumza na Mwandishi Diramakini mjini Morogoro kueleza nini atafanya pindi atakapoingia bungeni baada ya uchaguzi wa Oktoba.

Neema anasema, mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni lazima yapate msukumo mkubwa katika kuyaendeleza kwa lengo la kuzidi kutatua changamoto zinazowakabili watanzania, 

Neema anazitaja Asasi za Kiraia kama mdau mkubwa wa maendeleo hapa nchini huku akizitaja sera nzuri za serikali zinazochagizwa na utendaji madhubuti wa asasi hizo kuwa ni kiini kikubwa cha maendeleo ambayo Tanzania inayafikia.

ASASI ZA KIRAIA ALIZOTEMBELEA

Neema anasema kuwa, ametembelea asasi za kiraia 135 katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Morogoro huku akitarajia kutembelea asasi nyingine 60 katika Mkoa wa Kagera katika muda wa mwezi huu kabla ya uchaguzi.

Lugangira anasema kuwa, lengo la kutembelea asasi hizo ikiwa ni pamoja na kukutana na wakurugenzi wanawake ambao asasi zao zinashughulika na haki za wanawake na usawa wa kijinsia, kuwa ni kupata uelewa, kujua changamoto zilizopo ili kumwezesha kupanga vipaumbele vya kuanzia atakapoingia bungeni.

Anaeleza kuwa, kwa kuongea na wadau hao anapata fursa ya kupata mambo ya kujadili yaliyomo kwenye ilani ya CCM yanayohusiana na Asasi hizo na kuweza kubadilishana mawazo kwenye utekelezaji pamoja na kuwa kiunganishi bora kati ya Asasi, bunge, serikali, wafadhili na chama.

“Natumia kipindi hiki cha kampeni kukutana na wadau kutoka asasi za kiraia ili waweze kufahamu bungeni kuna hii nafasi, na kwamba CCM imetambua umuhimu wa Asasi hizo katika mchango wake kwa jamii na taifa kwa ujumla na ikaona itenge nafasi hii kwa ajli ya kutambua mchango wa asasi za kiraia katika maendeleo ya jamii,"anasema
 

Mbunge mteule viti maalum (CCM) kundi la Asasi za kiraia (NGOs) Tanzania Bara Neema Lugangira.
CHANGAMOTO ZA ASASI ZA KIRAIA

Neema anasema kuwa, katika kipindi alichotembelea asasi za kiraia amebaini changamoto nyingi zinazozikabili asasi hizo ambapo anaahidi atapambana kuhakikisha kuwa asasi hizo zinafanya kazi katika mlengo unaotarijiwa kwa ufanisi na ufasaha.

“Zipo changamoto nyingi ambazo asasi za kiraia zinakutana nazo katika utendaji wake wa kila siku, Changamoto hizo ni lazima zipatiwe ufumbuzi kwa ajili ya ustawi wa asasi hizo,"anasema Neema.

Neema anataja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni asasi nyingi za kiraia kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya sheria mpya ya NGOs, ambapo anapendekeza kuwa ni vema asasi zikawa zinapatiwa maelekezo na mafunzo maalumu pindi yanapotokea mabadiliko ya sheria ambazo zinahusu asasi hizo.

Anaitaja changamoto ya vigezo vya kupata ufadhili vinavyowekwa na wafadhili kwa asasi za ndani ambazo hupelekea miradi mingi kutekelezwa na asasi za kimataifa hali inayofanya baadhi ya miradi kutokuwa endelevu mara baada ya miradi kuisha.

“Kuna miradi mingine ambayo inatekelezwa na asasi za kimataifa ambazo ni muhimu na inatakiwa kuwa endelevu, sasa inapotokea miradi hiyo kufika ukomo na asasi hizo kuondoka nchini, asasi za ndani hushindwa kuendeleza miradi hiyo kutokana na kutotimiza vigezo vya ufadhili.” Anaeleza Lugangira.

Lugangira anasema kuwa kuna ushirikiano hafifu usiokidhi haja baina ya asasi za ndani kubwa na ndogo ambapo anapendekeza kuwa ni lazima ushirikiano huo uimarishwe kwa ajili ya ustawi wa asasi hizo na Taifa kwa ujumla.

Neema anasema kuwa ipo miradi ambayo inatekelezwa na asasi za kiraia ambayo haijielekezi moja kwa moja kwenye vipaumbele vya serikali zinazokidhi mahitaji ya jamii moja kwa moja na hivyo anashauri ni lazima asasi hizo zitekeleze miradi ambayo inashabihiana na vipaumbele vya serikali.

MIPANGO YAKE KUTATUA CHANGAMOTO HIZO

Neema anasema kuwa endapo atafanikiwa kuingia bungeni amejipanga kuwa kiunganishi muhimu kati ya asasi hizo na serikali huku akitaja njia atakazopendekeza kutatua changamoto hizo.

“Nitakuwa na vikao na makundi ya asasi za kiraia kutoka kwenye makundi na sekta tofauti maana kila sekta ina uhitaji wake kwa lengo la kubaini mahitaji ya kisekta na namna yanavyoweza kutatuliwa” Anasema Neema.

Neema anaongeza kusema kuwa sambamba na hilo atakuwa akifanya vikao vya mara kwa mara na wadau wa serikalini wa sekta tofauti ili kupata uelewa mpana wa nini uwe mchango wa asasi za kiraia.

Sambamba na hayo anasema kuwa atakuwa akifanya vikoa na kamati za bunge za kisekta na wawakilishi wa asasi zinazofanya kwenye sekta husika ili kwa pamoja wabaini namna bora ya kufanya kazi kwa tija.
Viongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) wakimsikiliza Mbunge Mteule Viti Maalum (CCM) Tanzania Bara, Neema Lugangira alipotembelea Mtandao huo mkoani Morogoro. (Diramakini).
“Nitaanzisha mipango ya kuzijengea uwezo asasi za ndani hasa zinazoongozwa na wanawake na ambazo zina mlengo wa kumuinua mwanamke na mtoto katika nyanja mbalimbali,"anasema.

Anaongeza kusema kuwa hatua hiyo itajumuisha pia asasi zinazolenga kuimarisha ushiriki wa wananwake kwenye nafasi za maamuzi na kisiasa.

USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI NA NAFASI ZA MAAMUZI

Neema anasema, kiwango cha wanawake wanaoshiriki katika kinyang’anyiro cha uchaguzi bado hakiridhishi, huku akisema idadi ndogo ya wanawake ambao wanashiriki katika uchaguzi iwe chachu ya kuwahamasisha wengine kujitokeza.

Hata hivyo anasema wanawake wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika vinyang’anyiro vya uchaguzi ili sera ya 50 kwa 50 katika vyombo vya maamuzi itimie.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news