Zaidi ya wajasiriamali 7,000 wamefikiwa na kupatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali yanayotolewa na Taasisi ya Openmind Tanzania katika Mkoa wa Dar es salaam, anaripoti Rachel Balama (Diramakini) Dar es Salaam.
Mafunzo yakiendelea jijini Dar es Salaam. (Diramakini).
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa mafunzo ya biashara kwa njia ya mtandao (digital marketing), Genoveva Mtiti kutoka katika taasisi hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wajasiriamali katika warsha iliyofanyika Ofisi za Jane Goodall Institute Mikocheni.
Amesema, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali hususani vijana lengo likiwa ni kuwakwamua katika lindi la umasikini kwa kuanzisha miradi mbalimbali.
"Tumeamua kutambua vijana na kuwapa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali hasa haya ya biashara mtandaoni ili waweze kufanya biashara zao kisasa zaidi kwa kutumia mitandao ya kijamii na kupanua wigo wa masoko,"amesema Mtiti.
Akizungumzia kuhusu mafunzo ya biashara mtandaoni, amesema yanatekelezwa katika nchi mbili za Tanzania na Kenya kwa kushirikiana na Jane Goodall Institute ambapo yameafadhiliwa na Fórum for International Cooperation (FIC).
Mafunzo yakiendelea jijini Dar es Salaam. (Diramakini).
Akitoa mada kwa wajasiriamali hao mwezeshaji kutoka Kampuni ya Akili Kubwa, Fredy Focus amesema katika Ulimwengu wa leo ni vema wafanyabiashara wanafanya biashara kwa kutumia njia za kisasa ili waweze kupata wateja wengi zaidi.
Amesema kuna njia mbili za kufanya biashara kidigitali ambazo ni njia za kisasa na za kizamani, lakini ili uweze kufanya biashara vizuri kwa kutumia mitandao ya kijamii ni vyema ukatumia njia ya kisasa ambayo ni kulipia gharama za matangazo kwenye mitandao ili bidhaa zitangazwe.