Profesa Sospeter Muhongo ambaye ni Mgombea Ubunge katika Jimbo la Musoma Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewaomba wananchi wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla wakipe ridhaa kwa kukichagua chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, kusudi kiweze kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na miradi ya kijamii pamoja na kulipaisha Taifa kiuchumi kama ilivyofanyika kwa miaka mitano ya Rais Dkt.John Magufuli,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini), Mara.
Amesema, kwa upande wake miradi ya maendeleo ikiwemo ya Elimu, Afya na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia fursa za Kilimo,Uvuvi na Ufugaji wenye tija amejipanga kwa kushirikiana na Serikali ya chama hicho kutekeleza kwa ufanisi.
Sambamba na kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) jimboni kwake ili vijana wafundishwe mbinu bora za ufugaji, uvuvi, ufundi, katika kutatua tatizo la ajira.
Ameyasema hayo Oktoba 8, mwaka huu wakati akinadi sera za Chama Cha Mapinduzi na kuomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Nyang'oma na Kwibara Kata ya Mugango Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, ambapo pamoja na mambo mengine Prof. Muhongo amesema CCM ndicho chama pekee nchini chenye uwezo wa kuendelea kulisukuma mbele Taifa na maendeleo ya wananchi wake.
"Jimbo la Musoma Vijijini tunaomba kura za mafiga matatu kwa sababu tunauhakika thabiti wa kutekeleza ilani kwa ufanisi tofauti na vyama vingine, tumeona Rais Magufuli ambavyo amefanya makubwa kwa miaka mitano Taifa limepiga hatua huu ni ukweli usiopingika naomba tena wananchi mkichague Chama Cha Mapinduzi kikazidi kufanya makubwa zaidi ya haya yaliyofanyika,"amesema Prof. Muhongo.
Ameongeza kuwa, upande wa elimu jimbo hilo lina shule 111 za msingi, kazi zilizofanyika kwenye elimu vyumba zaidi ya 400 vimejengwa kwa miaka mitano, na pia alitengeneza madawati 10,000, na kuyagawa katika shule za jimbo hilo ili watoto wasikae chini.Amesema, wanatakiwa kutengeneza takribani Madawati 3,000, kutokana na kuongeza kwa wanafunzi huku shule za msingi shikizi 11 zikiendelea kujengwa na baada ya uchaguzi wamejipanga kuchapa kazi ndani ya kata zote 21.
Amesema, katika Ubunge wake hatataka kuona watoto wakisomea chini ya miti, ambapo ndani ya miezi saba amejipanga vyema kufanya hivyo na kwa kushirikiana na madiwani wa chama hicho watakaochaguliwa, hivyo amewaomba wananchi wakichague CCM kwani vyama vingine, haviwezi kufanya hivyo, huku akisisitiza kila Shule ya Msingi katika Jimbo hilo ndani ya miaka 5 wanatarajia kujenga maktaba Watoto wajisomee kwa ufanisi ambapo vitabu atawezesha Prof. Muhongo katika Shule zote.
"Kwa miaka mitano tumeweza kusajili shule 3 ikiwemo Buringa Sekondari, Kwikuba Sekondari, Bugoji Sekondari, baada ya Uchaguzi narudi Busambara, Nyasaungu, tuendelee tena kujenga Sekondari zingine mpya na Halmashauri yetu imeamua tuongeze sekondari za kidato cha Tano na Sita, ambazo zimechaguliwa ikiwemo Bugwema Sekondari, Mtiro Sekondari, Mkirira Sekondari na Mugango Sekondari, nawaomba wananchi mchague madiwani wa CCM, Mbunge na Rais wakatekeleze haya kwa ufanisi mkichagua vyama vingine hawawezi kuyatekeleza haya,"amesema.