Rais Dkt.Ali Mohamed Shein awatunuku Kamisheni Maofisa wa Idara Maalum za SMZ

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewatunuku Kamisheni Maofisa wa Idara Maalum za SMZ na kuwapongeza kwa kufanikiwa katika mafunzo hayo.

Dkt.Shein amewatunuku Kamisheni hizo Maofisa hao huko katika viwanja vya Chuo cha KMKM Kama, Wilaya ya Magharibi A, katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mara baada ya kuwasili katika viwanja hivyo vya KMKM Kama, Rais Dkt.Shein alipokea salamu za heshima pamoja na kupokea gwaride kutoka kwa askari wa vikosi vya Idara ya SMZ.

Baada ya tukio hilo, Rais Dkt.Shein ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Idara Maalum za SMZ aliwatunuku Kamisheni Maofisa hao kutoka idara hiyo na baadae walikula kiapo cha utii.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri alitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dkt. Shein katika hafla hiyo pamoja na kumpongeza kwa kuiendeleza na kuilea vyema Idara Maalum za SMZ katika uongozi wake wote.

Waziri Kheri amesema kuwa, ndani ya miaka kumi ya uongozi wa Rais Dkt.Shein mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano yamepatika katika idara hizo Maalum za SMZ.

Nae Mwenyekiti wa Idara Maalum za SMZ,Commodore Hassan Mussa Mzee amesema kuwa, maafisa hao waliohitimu mafunzo hayo ni weledi, wachapakazi, jasiri, waaminifu na wazalendo kwa Serikali yao kutokana na mafunzo waliyoyapata.

Aidha, ameeleza kuwa, maafisa hao waliotunukiwa Kamisheni wako tayari kusimamia ulinzi, na usalama wa nchi yao sambamba na kuhakikisha hali ya amani na utulivu inaendelea kudumu hapa Zanzibar.

Kwa niaba ya maafisa hao, Commodore Mzee ametoa shukurani kwa Rais Dkt.Shein kwa uongozi wake bora na maelekezo yake mazuri kwa Idara Maalum za SMZ.

“Hakuna anayeweza kupinga kwamba katika uongozi wako Rais Dkt.Shein Idara Maalum za SMZ zimeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali,”amesema Commodore Mzee.

Mapema Mshauri wa Mafunzo ya Idara Maalum za SMZ, Meja Jenerali S.S.Omar alieleza namna ya mafunzo hayo yalivyotekelezwa kwa wahitimu hao wa mafunzo mbalimbali ambayo yameendeshwa huko katika chuo cha KMKM Kama pamoja na mafunzo yaliyoendeshwa katika chuo cha KVZ Pangatupu.

Meja Jenerali huyo alieleza kuwa mpango wa mafunzo uliotolewa na wizara hiyo unaelendea vizuri ambao tayari umeshaendesha kozi mbalimbali kwa mafanikio makubwa ambapo pia zipo nyingine zinatarajiwa kuendeshwa hapo baadae.

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali wa Serikali walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaey pia ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi na makamanda wa vikosi vya ulinzi vya SMZ na SMT na wanafamilia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news