Wagombea wawili wanaoshindania urais katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Novemba 3, mwaka huu nchini Marekani, Donald Trump wa Chama cha Republican na Joe Biden wa Democratic leo wanafanya kampeni katika majimbo ya katikati mwa nchi hiyo yenye ushindani mkubwa.
Aidha, janga la virusi vya corona (COVID-19) ambalo linazidi kuongezeka nchini humo ni kigezo kikubwa kinachotumiwa na wanasiasa hao kuomba kura.
Hata wakati ambapo Marekani imerikodi idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya virusi hivyo, Rais Trump anaendelea kubeza kitisho cha Covid-19, akisema anataka biashara ziruhusiwe kufanya kazi kama kawaida.
Naye Joe Biden ambaye ni makamu rais wa zamani, anamtuhumu Trump kutowajibika ipasavyo kupambana na janga hilo. Uchunguzi wa maoni ya wapigakura unamuonyesha Biden akiongoza kwa asilimia chache katika majimbo hayo, ambayo huenda yataamua mshindi.