Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli leo Oktoba 18, 2020 amemkabidhi nyumba mpya ya kuishi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,Ali Hassan Mwinyi iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania na kisha kukabidhiwa kwa Mhe.Rais Mstaafu Mwinyi kwa mujibu wa sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa namba 3 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2005 ambayo inaelekeza kuwa Marais wanapostaafu wanastahili kujengewa nyumba na Serikali.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt.Laurian Ndumbaro amesema ujenzi wa nyumba ya Rais Mstaafu Mwinyi ulioanza mwaka 2005 ulisimama kwa muda mrefu na baadaye mwaka 2018 uliendelea chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la Suma JKT kwa ushirikiano na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) hadi ulipokamilika.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo, Rais Mstaafu Mwinyi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msukumo mkubwa wa kukamilishwa kwa nyumba hiyo na ameishukuru Suma JKT na TBA kwa kujenga kwa ubora wa hali ya juu.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Mwinyi kwa kupata nyumba hiyo, na amemtakia heri na maisha mema katika makazi yake hayo mapya. Pia ameipongeza Suma JKT na TBA kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba maalumu ya Rais
mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete. Ujenzi wa nyumba hiyo
inajengwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria namba 3 ya Mwaka 1999
inayoainisha ujenzi wa nyumba maalumu kwa ajili ya makazi ya waheshimiwa
marais wanapostaafu. |
Wakati huo huo,Rais Magufuli amekagua jengo la nyumba ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete inayojengwa katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa nyumba hiyo ulianza mwaka 2018 chini ya TBA na Mhe. Rais Magufuli ameiagiza TBA kuhakikisha ujenzi wa nyumba, uzio na mandhali yake unakamilika ifikapo tarehe 30 Januari, 2021.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kujenga barabara ya lami yenye urefu wa meta 800 itakayounganisha nyumba hiyo na barabara ya lami iliyokaribu nayo.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiteta jambo na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne,Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipotembelea ujenzi wa nyumba ya Mhe.Kikwete inayojengwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria namba 3 ya mwaka 1999 inayoainisha ujenzi wa nyumba maalumu kwa ajili ya makazi ya waheshimiwa marais wanapostaafu.
Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ujenzi wa nyumba hiyo ambayo amesema anatarajia ndipo ataishi maisha yake yote.
Mapema leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamekwenda kumsalimu Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam.