Rais Shein afungua Skuli ya Sekondari ya Dk.John Pombe Magufuli jijini Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amewataka wazee kuendelea kusimamia malezi ya watoto wao, wakati huu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vikiwa vimeshamiri hapa nchini, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.

Dkt.Shein ametoa wito huo katika hafla ya ufunguzi wa Skuli ya Sekondari Mwanakwereke mpya, ambayo hivi sasa inatambulika kwa jina la ‘Skuli ya Sekondari ya Dk. John Pombe Magufuli.

Amesema, vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa vimeshamiri sio sifa ya Wazanzibari, hivyo akawataka wazee kote nchini kutoiachia serikali pekee jukumu la kukabiliana na uhalifu huo na badala yake kushirikiana nayo.“Hali hii ni lazima tushikamane katika kupambana na wahalifu hao,"amesema Rais Dkt,Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Kidato cha Tano wa Skuli ya Sekondari ya John Pombe Magufuli, Ahmada Hamid, skuli hiyo imepewa jina hilo baada ya kufunguliwa rasmi Oktoba 9, 2020 na kulia kwa Rais ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dkt. Idriss Muslim Hijja, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM,Dkt.Hussein Mwinyi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Riziki Pembe wakiwa katika chumba cha Maabara ya somo la Biaolojia. (IKULU).

Ameeleza kuwa, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wadogo, ikiwemo wanafunzi vimekuwa vikifanywa kwa makusudi, huku familia zinazoathirika zikiwaficha wahalifu wanaohusika na vitendo hivyo.

Dkt. Shein amesema, anaunga mkono kikamilifu azma ya Mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Mwinyi ya kuchukua hatua kali katika kukabiliana na vitendo hivyo, Rais amebainisha kuwepo matatizo ya kibinadamu, kiutawala na katika hulka za Wazanzibari katika ushughulikiaji wa vitendo hivyo.“Mambo yanayofanyika katika jamii yetu ni mabaya sana".

Rais Dkt. Shein amesema, Serikali inaendelea na juhudi za kuweka mazingira bora ya kielimu ili kupata wataalamu wazalendo na ndio maana skuli zinazojengwa kama hiyo zimekuwa na maabara za aina tofauti.

Ametoa wito kwa wanafunzi kusoma kwa bidii, huku serikali ikiendelea na jukumu lake la kuweka mazingira bora, ikiwemo kufanikisha dhana ya elimu bila malipo na kubainisha azma ya serikali ya kutoa elimu bure hadi kidato cha sita kadri uchumi utakavyoendelea kukua.

Amesema, Marehemu mzee Karume aliikomboa Zanzibar na hivi sasa mambo yote ya maendleeo yanafanywa na wananchi wenyewe.

“Nyinyi wanafunzi kazi yenu kusoma, serikali yenu iko pamoja nanyi na walimu nanyi somesheni kwa kutengeneza sio kulipua na wazee simamieni maendeleo ya elimu ya watoto wenu,"amesema, katika hatua nyingine, Dkt.Shein alipinga hoja zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa kiwango cha elimu kimeshuka nchini, na badala yake akasema kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu vizuri katika masomo yao, sambamba na kufahamu kuzungumza lugha za kigeni, hususan Kiingereza.

Amesema, walimu wanasomesha vizuri na bila ubaguzi huku idadi ya wanafunzi wanaohitimu idadi imekuwa ikiongezeka kutokana na ongezeko kubwa la wananchi kuzaliana kwa wingi.

“Kipimo cha elimu Zanzibar hakijashuka kuna wanafunzi wapatao 124 wa kidato cha sita ambao wamepata Divisheni ya kwanza, huku divisheni ya nne ikipungua na divisheni zero kufutika kabisa," amesema.

Amesema, mafanikio hayo yanachangiwa kutokana na mambo tofauti ikiwemo kiwango kikubwa cha Bajeti ya Fedha ya Wizara hiyo mwaka huu kinachofikia shilingi Bilioni 178, jambo ambalo kabla halikupata kutokea.

Aidha, Rais Dkt. Shein kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alikubali ombi la Uongozi wa Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali na kubariki skuli hiyo kuitwa jina la kiongozi huyo pamoja na kukubali skuli ya Sekondari Wingwi kuitwa jina lake (Dk. Ali Mohamed Shein).

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema Wizara hiyo itaendelea kusimamia maendeleo ya elimu nchini na kuhakikisha ubora wa elimu unasimamia vizuri.

Nae, Katibu Mkuu wa Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali,Mhandisi Dkt. Idrissa Muslim Hijja amesema hadi kufikia mwaka 2010 Zanzibar ilikuwa na jumla ya skuli 10 za Sekondari za ghorofa, ikiwemo Lumumba, Haile Sellasie, Ben-bella, Hamamni, Forodhani, Tumekuja, Uweleni, Kiponda, Hurumzi na Mwanakwerekwe ‘C’.

Amesema, katika kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wa Awamu ya Saba chini ya Dkt.Ali Mohamed Shein , jumla ya skuli 26 za Sekondari za ghorofa zimejengwa nchini kote.

Ameeleza kuwa, ufunguzi wa skuli hiyo sambamba na Skuli ya Sekondari Wingwi kisiwani Pemba, zinakamilisha jumla ya skuli 26 za Sekondari za ghorofa zilizojengwa katika Awamu ya Saba.

Amesema skuli hiyo iliyojengwa kupitia mradi wa Zanzibar Improving Students Prospects (ZISP) umegharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.6 hadi kukamilika kwake.

Amesema, lengo la mradi huo ni kuimarisha ubora wa elimu katika masomo ya Sayansi na Hisabati ngazi ya Sekondari na kuwapatia mafunzo ya somo la Kiingereza walimu wote wanaosemesha somo la Sayansi.

Aidha, amesema Kampuni ya Ujenzi ya CRJE kutoka nchini China ndio iliojengwa skuli hiyo,chini ya usimamizi wa kampuni ya ‘Digital Space Consultancy’.

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali wa kitaifa walihudhuria akiwemo Mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Sadalla,mawaziri pamoja na wanafunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news