_______________
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba
11 Oktoba 2020
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mgombea wa Kiti cha Rais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataendelea na ratiba ya Mikutano ya Kampeni katika Jiji la Dar Es Salaam kama ifuatavyo;-
Tarehe 12 Oktoba 2020
Mkutano Mkubwa utafanyika eneo la Kinyerezi Mwisho (Njiapanda ya kwenda Mitambo ya kufua umeme kwa gesi), katika Jimbo la Segerea na Wilaya ya Ilala. Wananchi wote na wana CCM mnakaribishwa na kuhamasishwa kufika mapema saa 2 asubuhi na Mkutano utaanza saa 3:00 Asubuhi.
Tarehe 13 Oktoba 2020
Mkutano Mkubwa utafanyika Uwanja wa Mburahati Barafu katika Jimbo la Ubungo na Wilaya ya Ubungo. Wananchi wote mnaombwa na kuhamasishwa kufika uwanjani saa 1 asubuhi na Mkutano utaanza saa 2 Asubuhi.
Tarehe 14 Oktoba 2020
Mkutano Mkubwa wa kufunga kampeni Jiji la Dar Es Salaam utafanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers. Wananchi wote wenye mapenzi mema na maendeleo katika Jiji la
Dar Es Salaam na wanachama wa CCM mnakaribishwa na kuhamasishwa kufika saa 2 asubuhi na Mkutano utaanza saa 3:00 Asubuhi.
Mikutano yote mitatu ratiba yake ina sehemu mbili, Sehemu ya kwanza ni Maelezo ya Utekelezaji wa Ilani ya 2015 – 2020 kutoka kwa wagombea ubunge wa CCM sambamba na kuomba kura, aidha sehemu hii ya kwanza inashereheshwa na vijana wana CCM wasanii wa muziki ambao pia watayaeleza mafaniko ya Awamu ya Tano kwa lugha ya Sanaa. Sehemu ya pili itaongozwa na Ndg. Magufuli mgombea wa Nafasi ya Rais kwa tiketi ya CCM ambaye atatueleza tulikotoka, tuliko na tunakokwenda, itakuwa fursa ya kuyasikia Maono yake kwa Dar Es Salaam na Taifa.
Taarifa ya ziada inatolewa kuwa siku ya tarehe 13 Oktoba 2020, Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atawaongoza Watanzania kupokea Mgao wa zaidi ya Bilioni 100 kutoka Kampuni ya Barrick Gold ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya kupitia upya Mikataba ya Madini na kutunga sheria zinazolinda madini na maliasili za Tanzania.
Tumetekeleza kwa Kishindo, Tunasonga Mbele kwa Pamoja
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI CHAMA CHA MAPINDUZI.