Serikali yahimiza kukamilishwa kwa wakati Kituo cha Kupoza Umeme Nyakanazi

Serikali imehimiza kukamilishwa kwa wakati, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nyakanazi ili pamoja na manufaa mengine, kiwaondolee wananchi wa Mkoa wa Kagera, adha ya kutokupata umeme wa kutosha,anaripoti Veronica Simba (WN) Ngara.

Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga alitoa maelekezo hayo jana, Septemba 30, 2020 kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo Kampuni ya L & T Construction kutoka India.
Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili-kushoto) na Ujumbe wake, wakikagua ramani ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi, walipozuru kituo hicho Septemba 30, 2020 kujionea maendeleo yake. (WN).
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi, wakiwa katika ziara ya kazi. (WN).

Akiwa amefuatana na Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Costa Rubagumya pamoja na Mhandisi Mkuu wa Nishati kutoka Wizarani, Salum Inegeja, alimtaka Mkandarasi kutumia mbinu mbalimbali zitakazomwezesha kukamilisha Mradi huo ifikapo Februari 2021, kama ilivyo kwenye Mkataba.

Mhandisi Luoga alibainisha kuwa kituo hicho kinategemewa na miradi mingine kadhaa ya umeme na kwamba pasipo ujenzi wake kukamilika, miradi hiyo pia haitaweza kuwanufaisha wananchi.
Kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi ikiendelea. Taswira hii ilinaswa wakati wa ziara ya Timu ya Serikali inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo, kukagua maendeleo ya utekelezaji wake, Septemba 30, 2020. Kituo hicho kinatarajiwa kukamilika Februari, 2021.(WN).
Meneja wa Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi Mhandisi Paschal Kibasa (kushoto) akionesha eneo kutakapojengwa kituo cha kupoza umeme Benaco, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera kwa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi. (WN).
Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa wataalamu wa kampuni ya ukandarasi ya JV WSP & GOPA INTEC, inayotekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi, akiwa katika ziara ya kazi. (WN).

“Mathalani, ili rradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Rusumo hadi hapa Nyakanazi, umbali wa kilomita 94, uweze kufanya kazi, unategemea Mradi huu wa kituo cha kupoza umeme ukamilike.”

“Pia, unahusisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Geita mpaka hapa Nyakanazi, umbali wa kilomita 54,” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu manufaa ya kituo hicho, alisema kikikamilika kitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera ambayo itaingizwa katika gridi ya Taifa kama alivyoagiza Rais John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa tafsiri ya uwepo wa umeme wa uhakika inamaanisha shughuli za kijamii na kiuchumi zitaboreshwa hivyo Pato la Taifa litaongezeka. Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi Mhandisi Paschal Kibasa (kulia), wakati wa ziara ya kazi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo. Kushoto ni Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Salum Inegeja. (WN).
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi. Timu hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi. (WN).
Kutoka kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Costa Rubagumya, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi kutoka NELSAP, Gaspar Mashingia pamoja na Mhandisi Mkuu wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Salum Inegeja wakiwa katika ziara ya Timu ya Serikali (wengine hawapo pichani) kukagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi. (WN).
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo, wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti na wafanyakazi wa Kampuni ya Ukandarasi L & T Construction inayotekeleza Mradi wa Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi. Timu hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi. (WN).
Alieleza manufaa mengine ya kukamilika kwa kituo hicho kuwa ni kuwezesha biashara ya umeme baina ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Rwanda na Burundi kwani kituo hicho kitaunganishwa na kituo cha Rusumo, ambacho Mradi wake wa kuzalisha umeme unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo tatu.

Kuhusu mbinu ambazo alishauri Mkandarasi azitumie kukamilisha kazi kwa wakati, Mhandisi Luoga alizitaja kuwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi pamoja na kuongeza muda wa kufanya kazi.

Pamoja na kutoa maelekezo hayo, Mhandisi Luoga alikiri kuwa yeyé pamoja na wenzake alioambatana nao wameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi huo hivyo akampongeza Mkandarasi husika kwa utendaji mzuri.

Kwa upande wake, Mkandarasi huyo alimhakikishia Mhandisi Luoga na Ujumbe wake kuwa kampuni yake imejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na viwango stahiki ili kutunza rekodi yao ya utendaji kazi mzuri inayotambulika duniani kote.

Awali, Timu hiyo ya wataalamu kutoka serikalini ilikagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) kutoka Rusumo hadi Nyakanazi, wakiwa wameambatana na Meneja wa Mradi husika, Mhandisi Paschal Kibasa ambapo walishuhudia kazi za awali za utekelezaji zikiendelea kwa kasi.

Aidha, Timu hiyo ilikagua eneo kutakapojengwa kituo cha kupoza umeme Benaco ambacho kitapeleka umeme Kyaka hivyo kuwezesha kuunganisha Mkoa wote wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa.

Timu hiyo ya Serikali imekamilisha ziara yake ya siku tatu wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, ambayo ilihusisha kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera (megawati 80), ukizijumuisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news