Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetaka taarifa inayosambaa mitandaoni juu ya watu waliofanya kazi kati ya mwaka 1990 hadi 2020 kuwa kuna malipo ya mafao yao ipuuzwe, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama leo Oktoba 12,2020.
"Ndugu wananchi, ninapenda kuwajulisha kuwa katika siku za karibuni kumekuwepo na taarifa ambazo zinaenea katika mitandao ya kijamii kuwa kuna malipo ya mafao yanayotolewa na Wizara ya Kazi kwa watu waliofanya kazi kati ya mwaka 1990 hadi 2020.
"Kupitia mitandao hiyo, imeelezwa kuwa wafanyakazi hao wana haki ya kupata mafao ya kiasi cha shilingi 3,500,000. Ninanukuu taarifa hiyo “Those who worked between 1990 and 2020 have the right to withdraw 3,500.000 shilling from Ministry of Labour Tanzania.To check your eligibility visit sroht.com/labour/tz”.
"Ninaomba nitumie fursa hii kuutangazia umma kuwa taarifa hiyo haina ukweli na hivyo ipuuzwe. Aidha,ninawataka wahusika kuacha mara moja kuendelea kusambaza taarifa hiyo.Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao endapo watakaidi maelekezo haya,"amefafanua Waziri Mhagama.
Tags
Habari