Shura ya Maimamu kwa kushirikiana na Baraza Kuu, Taasisi na Jumuiya za Kiislam zimevitaka vyombo vya dola kuwashughulikia pasipo upendeleo viongozi wa dini hususani ya Kiislam watakaosimama kwenye majukwaa ya kisiasa kunadi wagombea ili kunusuru Taifa,anaripoti Rachel Balama (Diramakini), Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 20,2020 kwa niaba ya Mkuu wa Shura ya Maimamu Mjumbe wa Shuraa hiyo, Sheikh Juma Ramadhan Juma amesema, sasa imejitokeza tabia ya viongozi wa dini si mara moja kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa na kuwataka watu wamchague kiongozi fulani jambo ambalo linaweza kuleta athari.
Amesema kuwa, viongozi wa dini hawapaswi kusimama katika majukwaa ya siasa na kuwanadi wagombea na badala yake wawaachie wanasiasa wenyewe na kwamba wananchi ndio wataamua kwenye masanduku ya kura.
Amesema, hakuna kikao chochote kilichokubaliana kwamba Waislam wampigie kura mgombea fulani na kutaka masuala hayo waachiwe watanzania wenyewe ndio wataamua nani anafaa kuwa kiongozi wao si vingine.
"Kwa niaba ya Shura ya Maimamu, naomba Jeshi la Polisi kuwashughulikia viongozi wa dini hasa ya Kiislam wanaosimama kwenye majukwaa ya kisiasa iwe ya CCM au ya upinzani ili kuepusha kuhatarisha amani,"amesema.
Amesema, hakuna sehemu yoyote viongozi wa dini hiyo walikutana na kukubaliana wamchague mgombea fulani na kwamba huo ni utashi wao binafsi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuwagawa waumini wao.
Aidha, amelitaka Jeshi la Polisi kuwashughulikia viongozi wa dini watakaosimama kwenye majukwaa ya kisiasa kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kulinusuru Taifa dhidi ya uvunjifu wa amani.
Amesema, kitendo alichofanya Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salam Alhad Musa Salum pamoja na mwana chama wao Sheikh Issa Ponda si vya kufumbiwa macho.
Amesema kuwa, Waislamu wana jambo lao kubwa ambalo ni vizuri wakalijadili kwa undani nalo ni ndugu zao ambao wapo Gerezani kwa kipindi cha miaka nane sasa kwa tuhuma za ugaidi, lakini sio la kuwachagulia mgombea.
"Waislam wajikite kuangalia ndugu zao masheikh ambao wako Gerezani mwaka wa nane sasa kwa tuhuma za ugaidi na hawajui hatma yao na mbaya zaidi wana familia ambazo zinawategemea,"amesema.
Amesema kuwa, wanasubiri Sheikh Issa Ponda atakaporudi viongozi watakaa na kuzungumza naye kisha uongozi utatoa taarifa.