Simba SC ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wamezinduka kutoka kwenye vipigo viwili mfululizo baada ya kuichapa Mwadui FC mabao 5-0 jioni ya leo Oktoba 31,2020 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo wa kwanza katika mechi tatu, unaifanya Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ifikishe alama 16 baada ya kucheza mechi nane na kurejea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam FC na Yanga wenye alama 22 kila mmoja.
John Raphael Bocco ambaye ni nahodha na mshambuliaji wa timu hiyo, leo amefunga mabao mawili katika ushindi huo, bao la keanza 25' akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama na la pili 64' akimalizia kazi nzuri ya mtokea benchi Hassan Dilunga.
Naye kiungo wa zamani wa Yanga SC, Hassan Dilunga amefunga mabao mawili, la tatu 81' akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake, Ibrahim Ajibu na la nne dakika ya 86 akimalizia pasi ya Said Ndemla.
Ndemla ambaye amerejea kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC msimu huu baada ya kusota benchi kwa muda mrefu msimu uliopita akakamilisha shangwe za mabao kwa wana Msimbazi baada ya kufunga bao la tano 90'.
Ushindi huo ni ahueni kwa mabingwa hao wa watetezi, kufuatia kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita zote wakichapwa 1-0 na Tanzania Prisons huko Sumbawanga mkoani Rukwa na Ruvu Shooting hapa Dar es Salaam.
Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa kimeundwa na Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein (Tshabalala), Joash Oyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Rally Bwalya/Hassan Dilunga 60', Said Ndemla, John Bocco/Ibrahim Ajibu 70', Clatous Chama/ Fransis Kahata 85' na Luis Miquissone.
Kwa upande wa Mwadui FC kilikuwa kimeundwa na Mussa Mbisa, Jackson Shiga/Lilan Hussein 67', Shaaban Kingazi, Halfan Mbarouk, Joram Mgeveke, Abbas Kapombe, Abubakar Kambi, Enrick Nkosi, Deogratius Anthony, Ismail Ally na Herman Masenga/Msenda Amri 77'.
Wakati huo huo Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Biashara United jioni ya leo Uwanja wa Karume uliopo Musoma mkoani Mara.
Ushindi huo wa saba mfululizo katika mchezo wa nane wa msimu, unaifanya Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze ifikishe alama 22, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa wastani wa mabao na Azam FC ambayo hata hivyo imecheza mechi moja zaidi.
Bao pekee la Yanga SC leo limefungwa na mshambuliaji wake Mghana, Michael Sarpong 68' akimalizia krosi ya Ditram Nchimbi kutoka upande wa kulia.
Kikosi cha Biashara United kilikuwa kimeundwa na Daniel Mgore, Mushta Batozi/Geeshon Samuel 86', Mpapi Salum, Lenny Kissu, Abdulmajid Mangaro, Hamad Tajiri, Deogratius Judika, Kauswa Bernard, Gerlad Mathias/ Kelvin Friday 67', Omary Nassor/ Ramadhan Chombo (Redondo) 46' na Tariq Simba.
Aidha kikosi cha Yanga SC kiliundwa na Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Adeyoum Ahmed, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Ditram Nchimbi/ Yacouba Songne 82', Feisal Salum/ Zawadi Mauya 88', Michael Sarpong, Waziri Junior/Tuisila Kisinda 60' na Farid Mussa.
Wakati huo huo Namungo FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, bao pekee la Steven Sey dakika ya 66 Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.
Mechi nyingine Polisi Tanzania FC wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons FC bao pekee la Marcel Kaheza kwa penalti 53' Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga mkoani Rukwa.