Naibu Waziri wa Kilimo,Omary Mgumba. |
Ndugu Wananchi,
Tarehe 16 Oktoba ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi wanachama wenzake wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika kusherehekea Siku ya Chakula Duniani.
Chimbuko la Siku hii ni Mkutano wa mwaka 1979 ambapo nchi wanachama wa FAO zilikutana Jijini Quebec nchini Canada na kujadili kiundani masuala mbalimbali kuhusu chakula. Mojawapo ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa kutenga siku moja ya kila mwaka ili kuzungumzia na kutafakari njia na mbinu mbalimbali za kupata chakula cha kutosha kwa watu wote duniani na kwa wakati wote.
Maadhimisho ya kwanza ya siku hii yalifanyika mwaka 1981. Hivyo maadhimisho ya mwaka huu ni ya 40 na yanasherehekewa kwa pamoja na maadhimisho ya miaka 75 ya kuanzishwa kwa FAO tarehe 16 Oktoba, 1945.
Kwa wakazi wa mkoa wa Njombe na mikoa jirani ya Nyanda za Juu Kusini nawaomba mjitokeze kwa wingi kwenye maadhimisho haya ambayo yatazinduliwa rasmi kitaifa tarehe 10/10/2020 na kufikia kilele chake tarehe 16 Oktoba, 2020 mkoani Njombe.
Ndugu Wananchi,
kila mwaka Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) huchagua kaulimbiu ambayo huwa inatoa dira ya kuhamasisha wadau wote wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuchangia katika kuhakikisha kila mtu anawezeshwa kupata chakula bora na cha kutosha wakati wote wa maisha yake.Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema ‘ Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu”
Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kutekeleza kauli mbiu hii kwa kuhakikisha uzalishaji wa chakula nchini unaimarika na kutosheleza mahitaji ya chakula. Hali ya chakula mwaka huu ni nzuri,kutokana na uzalishaji mzuri katika msimu wa 2019/2020.
Tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya uzalishaji kwa msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14,347,955. Mahitaji haya yakilinganishwa na uzalishaji nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3,511,620 za chakula ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka.Kiwango hiki cha uzalishaji kimeiwezesha nchi kutosheleza mahitaji yake ya chakula kwa kiwango cha utoshelevu ( Self Sufficient Ratio-SSR ) cha asilimia 124.
Aidha, uzalishaji wa mahindi na mchele unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 6,388,446 na 2,942,895 mtawalia. Kwa ulinganifu wa mahitaji mahindi na mchele kwa nchi ambayo ni kiasi cha tani 5,737,132 za mahindi na tani 1,087,646 za mchele, nchi inatarajiwa kuwa na ziada ya tani 651,314 za mahindi na tani 1,855,249 za mchele.
Ndugu Wananchi
Pamoja na kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula bado hali ya lishe nchini si nzuri japokuwa kuwa taarifa zinaonyesha kuna maendeleo mazuri katika kupunguza utapiamlo. Takwimu zinaonesha kuwa udumavu umepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2018. Ukondefu umepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018 ambayo ni chini ya kiwango cha malengo ya Mkutano wa Afya Duniani (WHA) cha asilimia 5. Pamoja na mafanikio haya bado idadi ya watoto wenye udumavu ni kubwa mno (zaidi ya milioni 3) hali ambayo haikubaliki. Aidha bado tunakabiliwa na utapiamlo unaotokana na ukosefu/upungufu wa virutubishi mwilini ambavyo ni Vitamini na Madini kama vile madini chuma, madini joto (Iodine) na Zinki.
Hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa kwa jamii nyingi kutotambua umuhimu wa kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula ili kuwa na afya bora. Hali hii imedhihirika wazi kwani takwimu zinaonesha kuwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi ndiyo yenye viwango vikubwa vya udumavu kwa watoto kwa mfano Njombe asilimia 53.6, (Uzalishaji tani 446,491;kiwango cha utoshelevu- SSR% 194) Rukwa asilimia 47.9, (Uzalishaji tani 943,002;kiwango cha Utoshelevu-SSR% 230) Iringa asilimia 47.1,(Uzalishaji tani 470,750;kiwango cha utoshelevu-SSR% 161) Songwe asilimia 43.3, (Uzalishaji tani 805,545;kiwango cha utoshelevu-SSR% 210), Kigoma asilimia 42.3 (Uzalishaji tani 1,158,214; kiwango cha utoshelevu –SSR% 165);na Ruvuma asilimia 41.0,(Uzalishaji tani 1,251,511;kiwango cha utoshelevu-SSR% 237).
Ndugu Wananchi
Sote ni mashahidi kwamba kazi kubwa imefanyika katika kupunguza hali hii duni ya lishe. Serikali kwa mfano, imendaa na inatekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multsectoral Nutrition Action Plan- 2016/2017- 2020/2021) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII). Mikakati hii ya kitaifa imeainisha majukumu ya wadau mbalimbali katika kuchangia kupunguza lishe duni nchini.
Wizara yangu inajukumu la kuhakikisha mazao mbalimbali ya chakula na hasa yenye virutubishi kwa wingi kama vile mboga na matunda na mazao yaliyoongezewa virutubishi kibaiolojia kama vile viazi lishe, mahindi lishe na maharage lishe yanazalishwa kwa wingi na kusindikwa na hatimaye yanaandaliwa na kutumiwa ipasavyo ili kumpatia mlaji afya bora. Aidha Wizara inaendelea kuboresha miongozo mbalimbali na kutoa elimu ya namna ya kuzalisha, kuhifadhi na kutumia mazao ya mikunde kama vile Soya,Choroko,Mbaazi na Dengu ambayo yana viini lishe aina ya protini kwa wingi na kupatikana kwa gharama nafuu.
Ndugu Wananchi
Katika kutekeleza hilo, hivi karibuni Wizara yangu ilizindua Mwongozo wa kuongeza virutubishi kibaiolojia katika mazao ya chakula na Mwongozo wa kutekeleza masuala ya lishe katika kilimo ambayo ilizinduliwa na Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika maonesho ya wakulima Nanenane Mkoani Simiyu. Pia Wizara yangu inaandaa Mpango wa kutekeleza masuala ya lishe katika kilimo kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo (FAO) ambao utaelekeza wadau wa kilimo kote nchini kutekeleza masuala ya lishe na hivyo kuchangia katika kupunguza utapiamlo na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni pamoja na: -
Kuwawezesha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kujifunza teknolojia sahihi za kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kupata chakula bora na cha kutosha kwa kila mtu na kwa wakati wote;
1:Kuongeza jitihada na mbinu za kutokomeza njaa, utapiamlo na hatimae kuondoa umaskini;
2:Kuainisha mikakati thabiti ya kuhakikisha kila mtu anapata chakula bora na cha kutosha wakati wote;
2:Kuelimisha wananchi kuondokana na mila potofu zinazozuia baadhi ya jamii kula aina fulani za vyakula, kwa mfano kutokula mayai kwa akina mama wajawazito.
3:Kuimarisha Ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa katika masuala ya kukuza na kuendeleza kilimo, ufugaji na uvuvi;
4:Kuelezea kihistoria nafasi ya mila na utamaduni katika kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji.
Ndugu Wananchi
Wakati wa maadhimisho hayo; shughuli zifuatazo hufanyika ili kufikia malengo na madhumuni yaliyoorodheshwa hapo juu: -Maonesho ya kazi mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji, tija na upatikanaji wa chakula na usindikaji wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi;
1:Kutoa elimu juu ya kuandaa vyakula mbalimbali, lishe bora, uhifadhi na usindikaji wa mazao ya chakula, mifugo na uvuvi katika ngazi ya kaya na jamii.
2:Kutoa elimu ya Usalama na Uhakika wa chakula na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa.
3:Kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwa na ufahamu wa umuhimu wa lishe bora na ujuzi wa kuandaa mlo kamili.
4:Kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya vyakula vya asili katika ngazi ya kaya na jamii.
Hotuba na maelekezo ya Viongozi mbalimbali (Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa);
Ndugu Wananchi
Kabla ya kuhitimisha tarifa yangu hii ,napenda kutoa shukrani zangu kwa niaba ya Wizara ya Kilimo kwa wadau hawa waliofanikisha maandalizi ya maadhimisho ya mwaka huu .Nao ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO),Shirika la Chakula Duniani (WFP) na taasisi, Idara na sekta binafsi ambao wameridhia kushiriki kwenye maadhimisho haya.
Kwa taarifa hii naomba Viongozi na Wananchi wote kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ya Siku ya Chakula Duniani nchini kote.
OMARY TEBETWE MGUMBA
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA KILIMO
Tarehe 01 Octoba, 2020