TAKUKURU GEITA YANG'ATA ALIYEKOPESHA MWALIMU MSTAAFU MKOPO WA RIBA YA ASILIMIA 900

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imefanikiwa kurejesha shilingi milioni 5,500,000 ambazo zilikuwa zimechukuliwa na Isack Nyamhanga kutoka kwa mwalimu mstaafu Adela Faustine kwa kumkopesha shilingi laki saba na kumlazimisha alipe milioni saba baada ya kugundua amelipwa kiinua mgongo baada ya kustaafu,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini), Geita.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix (kulia) akimkabidhi shilingi milioni 5,500,000 Bi. Adela Faustine Mwalimu mstaafu zilizookolewa kutoka kwa mfanyabiashara, Isack Nyamhanga aliyekuwa amechukua milioni 7 kwa mkopo wa laki 7 tu. (Diramakini).
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix amesema kuwa, Mwalimu huyo alikopa Laki Saba kutoka kwa mfanyabiashara huyo, lakini baada ya kupata taarifa kwamba pensheni yake imeingia kwenye akaunti akaanza kumpa vitisho na kumlazimisha amlipe milioni saba.

Felix amesema kuwa, Adela alilipa kiasi hicho kwa Isack Nyamhanga ambacho ni sawa na asilimia 900 ya mkopo huo ambao ulikuwa kinyume na sheria za uendeshaji shughuli za fedha nchini.

Amefafanua kuwa, baada ya mwalimu huyo mstaafu kutoa taarifa Takukuru, taasisi hiyo ilifuatilia na kumbana na kufanikiwa kurejesha milioni 5.5 na kiasi kingine atakirejesha baadae.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix amesema kuwa, baada ya kumfanyia upekuzi mfanyabiashara huyo alikutwa na kadi za benki ambazo ni mali za watumishi mbalimbali wa umma 64 ambazo ni za wakopaji ambao wanampatia pia namba zao za siri zilizosajiliwa benki.

Amewaomba wananchi na watumishi wa umma kuacha kushiriki katika mikopo umiza hiyo kwa sababu kufanya hivyo ni kushiriki kutenda jinai, lakini ni kudhalilisha pia utumishi umma.

Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa TAKUKURU kwa wale ambao wamefanyiwa mikopo umiza ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wafanyabiashara wote wanaofanya biashara ya kutoa mikopo hiyo ambayo ni kinyume cha sheria za nchi.

Kwa upande wake, Adela Faustine amesema kuwa, alichukua mkopo kutoka kwa Isack Nyamhanga laki saba na alidumu na mkopo huo miezi sita tu.
Bi.Adela Faustine Mwalimu mstaafu akionyesha kiasi cha shilingi milioni 5,500,000 baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix zilizookolewa kutokana na mkopo umiza wa riba ya asilimia 900. (Diramakini).
Anasema, baada ya miezi hiyo alilipwa pensheni yake na alipoenda kulipa deni mhusika alimbadilikia na kumlazimisha kwa vitisho alipe kiasi kikubwa zaidi cha milioni saba.

Ameeleza kuwa,alilazimika kulipa fedha hiyo kwa sababu alikuwa hajui ni mamlaka ipi inaweza kuingilia kati kumaliza tatizo hilo.

Anasema, hivi karibu alipata wazo la kwenda TAKUKURU na alipofika amesaidiwa ndani ya siku 14 fedha zake zilikuwa zimerudishwa.

Pamoja na kuondoa fedha hizo, TAKUKURU Mkoa wa Geita katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka huu,imeokoa jumla ya 191,198,624.92 zilizokuwa zimefanyiwa ubadhirifu kwa njia mbalimbali za rushwa na dhuluma.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix akionyesha baadhi ya kadi za benki mbalimbali za watumishi wa umma zilizokutwa kwa mfanyabiashara, Isack Nyamhanga zinazoachwa kwake baada ya kupokea mikopo umiza. (Diramakini).
TAKUKURU imeokoa kiasi cha Shilingi 13,194,323 za Geita SACCOS, shilingi 16,630,000 za Chama cha Ushirika cha Wachimbaji wadogo cha Ikuzi wilayani Bukombe na shilingi 300,000 za SACCOS ya Katoma.

Fedha nyingine ni 1,527,000 za mishahara hewa sekta ya elimu,1,309,600 ambazo ni posho za waandishi wa habari,25,992,000 zilizotozwa kwa wananchi maeneo mbalimbali kwa njia ya dhuluma,hongo na michango iliyo kinyume na sheria.

Kiasi kingine ni 2,601,000 za manunuzi hewa serikali za mitaa,4,044,000 deni la wakulima wa pamba waliokuwa wamedhulumiwa na wahasibu wa Amcos za Nyamigogo na Nyamalimbe.

Nyingine ni 69,690,000 zilizotokana na biashara haramu ya mkaa uliokamatwa na Takukuru na kisha kupigwa mnada na fedha hizo kulipwa serikali kwa Wakala wa misitu nchini (TFS).

Aidha, TAKUKURU pia imetemesha 47,967,307.92 ambazo ni kodi ya huduma ya Halmashauri ya Mji wa Geita kutoka kwa Nyamatagata SACCOS ambayo inafanya biashara ya vyuma chakavu kutoka Mgodi wa kuchimba Dhahabu wa Geita (GGML) pamoja na 7,943,400 malipo ya fidia kwa wananchi kwa ajili ya mashamba yao kwa eneo la Nyankumbu kutokana na kupisha ujenzi wa barabara ya lami ya Geita-Bwanga-Biharamulo mwaka 2005/2008.

Aidha,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Leonidas Felix amewaomba wananchi katika kipindi hiki cha uchaguzi kujiepusha na vitendo vya rushwa kama kusafirishwa kwenda kupiga au kula chakula au vinywaji kwa mgombea siku baada kutangazwa mahindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news