Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) makao makuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) imewafikisha mahakamani watuhumiwa wanne kwa tuhuma za rushwa, uhujumu uchumi, kuisababishia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari hasara ya shilingi 619,278,260.52 pamoja na ukwepaji kodi wa shilingi 37,837,409.26, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 12, 2020 na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU, Doreen J.Kapwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo. Amesema, kati ya watuhumiwa watatu walikuwa ni watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa tayari wameshafukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Kapwani amesema, mwingine ni mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya M/S Ntinyako Company Limited iliyokuwa ikipewa zabuni ya usambazaji wa vifaa vya ujenzi na miundombinu ya maji katika Ofisi ya Bandari Kigoma.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Kenneth Mtembei washitakiwa wanakabiliwa na Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 5/2020.
Kesi yao inahusisha makosa ya: - 1. Kuongoza genge la uhalifu kinyume na Aya ya 4(1)(d) ya Jedwali la Kwanza likisomwa pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) Vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo mwaka 2002.
2. Ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa No.11/2007.
3. Kuisababishia Mamlaka Hasara Kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza likisomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) Vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo mwaka 2002.
4.Kushindwa kulipa kodi kinyume na kifungu cha 83(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi Namba 10 ya Mwaka 2015. Na
5. Kutakatisha fedha Kinyume na kifungu cha 12(a) na 13(a) Cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha No. 12 ya Mwaka 2006 ikisomwa pamoja na Aya ya 22 ya Jedwali la Kwanza la vifungu vya 57(1) na 60(2) Vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo Mwaka 2002.