Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga imeokoa zaidi ya shilingi milioni 214,760,327.00 za Serikali pamoja na wananchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala ameyabainisha hayo leo Oktoba 15, 2020.
"Ndugu wanahabari nimewaita hapa leo ili nizungumze na wananchi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla kupitia ninyi wanahabari kwa lengo la kuujulisha umma juu ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2020.
"Huu ni utaratibu ambao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa tumejiwekea ili Watanzania waweze kufahamu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na TAKUKURU katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
"Kwa ujumla na kwa ufupi nitazungumzia kazi zilizofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2020 na pia mikakati yetu katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2020 ikiwemo kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.
"Tunafanya hivyo pia ili kutekeleza matakwa ya Katiba, kwa maana ya kuwapa wananchi fursa na haki yao ya kupewa taarifa kuhusu matukio mbalimbali nchini, kama ilivyoelezwa katika ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake.
"Nianze na jukumu letu TAKUKURU la kuelimisha umma. Kwa mujibu wa kifungu cha 7(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, TAKUKURU inalo jukumu la kuhimiza na kuendeleza uungaji mkono wa jamii katika kupambana na vitendo vya rushwa. Jukumu hili hutekelezwa kupitia Dawati la Elimu kwa Umma.
"Katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2020 TAKUKURU Mkoa wa Tanga tumeelimisha umma kwa kuendesha semina 77, mikutano ya hadhara 78, Ufunguzi wa klabu mpya 15 za wapinga rushwa na uimarishaji klabu 71 za wapinga rushwa zilizopo katika shule na taasisi mbalimbali mkoani Tanga, sambamba na kuandaa habari na makala nane,"amefafanua.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala amefafanua kuwa, TAKUKURU Mkoa wa Tanga pia wamefanya vipindi vya redio 24 kupitia vituo vya redio vilivyopo mkoani Tanga.
"Lakini pia kutoa taarifa tano kwa umma kupitia vyombo vya habari vilivyopo mkoani Tanga na nitumie fursa hii kuwashukuru walimiki wa vyombo hivyo pamoja na wafanyakazi wao wote kwa kuwa sehemu ya kufanikisha hilo, kwani mmekuwa mkiitika kila tulipo waita, Ahsanteni sana.
"TAKUKURU Mkoa wa Tanga tunahamasisha na kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa tukiamini kwamba wananchi wakiwa na uelewa kuhusu rushwa watachukua hatua ya kutoa taarifa, kukemea na kushirikiana na Serikali kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya rushwa.
"Ndugu wanahabari kuhusiana na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na udhibiti. Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2020, TAKUKURU Mkoa wa Tanga kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Serikali, imefanya ufuatiliaji wa miradi 17 ya maendeleo katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni 12,483,670,042.72.
Miradi iliyofuatiliwa ni katika sekta za ujenzi, barabara, elimu na maji. Sambamba na miradi ya Maendeleo TAKUKURU Mkoa wa Tanga pia imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Serikali zinazotengwa kwa matumizi mbalimbali katika ofisi za Serikali na taasisi za umma.
Ufuatiliaji huu hufanyika kwa kufuatilia mtiririko wa fedha kutoka chanzo (Hazina, Wafadhili au Vyanzo vya ndani) mpaka mahali fedha zilipolengwa kutumika. Aidha ndani ya miezi mitatu umefanyika uchambuzi wa mifumo 10, warsha tatu na ufuatiliaji wa maazimio mawili mkoani Tanga.
Dawati la Sheria na Mashtaka
Kwa mujibu wa Kifungu cha 7(e) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 7 ya mwaka 2007, ni jukumu la TAKUKURU kuchunguza au kupeleleza na kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuendesha kesi mahakamani kwa kuwashitaki watuhumiwa wote wanaotuhumiwa kutenda makosa chini ya sheria hii na makosa mengine yanayohusisha Rushwa.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala amesema, katika kutekeleza jukumu hilo, ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Tanga imepokea jumla ya taarifa 268 za vitendo vya rushwa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2020.
"Mchanganuo wa taarifa hizo kiidara unaonyesha kwamba Idara ya Afya 3, Utawala 10, fedha 8, ujenzi 12, Madini 5, Misitu 9, Mifugo 5, biashara 3, Halmashauri za Wilaya na Miji 27, Mahakama 24, Elimu 23, Mirathi 16, Kilimo 2, Michezo 1.
"Idara zingine zilizolalamikiwa ni pamoja na Magereza 1, na Jeshi la Polisi 11, Vyama vya ushirika 8, SACCOS 2, VICOBA 4, NGO 1, Taasisi za Dini 1, Vyama vya Siasa 9, Mashirika ya Hifadhi ya Jamii 16, Tanesco 2, Uhamiaji 2, TANROADS 3 na taarifa zinazohusu watu binafsi 33,"amefafanua
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala.
Aidha, amesema baada ya kuzifanyia uchunguzi wa awali taarifa tajwa, taarifa 159 ziligundulika kwa ni za vitendo vya rushwa na taarifa 109 hazikuwa zinahusiana na vitendo vya rushwa. "Jumla ya taarifa 80 zimefungwa baada ya watoa taarifa kushauriwa na baadhi kuelekezwa kwenda idara husika na taarifa 188 zinaendelea kuchunguzwa.
"Kwa upande wa uendeshaji mashitaka TAKUKURU Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2020, imeendesha jumla mashauri 16 Mahakamani ambapo mashauri 13 yalifunguliwa kabla ya Julai 2020 na mashauri 03 ni kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2020.
"Aidha, kati ya kesi hizo 16 zilizoendeshwa mahakamani kesi tano zilitolewa hukumu ambapo watuhumiwa watano walikutwa na hatia na watuhumiwa wa kesi mbili waliachiwa huru kama ifuatavyo,
"Kesi yenye Na. Corr. Case 2/2019 watuhumiwa wamehukumiwa kila mmoja kulipa faini ya Shilingi 1,000,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela na wamelipa faini kukwepa kifungu. Kesi Na. CC. 49/2019- mtuhumiwa alihukumiwa kwa makosa tisa kulipa faini ya shilingi 6,000,000 au kifungo cha miaka 10 jela ambapo mtuhumiwa alilipa faini na kukwepa kifungu.
"Pia kesi Na. CC 25/2018 ambapo mshtakiwa amelipa faini ya shilingi 200,000. Katika kesi Na. ECC. 17/2018 watuhumiwa walikuwa watatu wawili waliachiwa huru na mmoja alitiwa hatiani, hata hivyo aliyetiwa hatiani ni marehemu.
Aidha, katika kesi Na. CC 04/2018 watuhumiwa waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu na kesi Na. CC 05/2018 pia watuhumiwa waliachiwa huru,"amefafanua Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala .
Pia amesema, TAKUKURU Mkoa wa Tanga katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba, 2020 imeweza kuokoa jumla ya shilingi 214,760,327.00 ambazo ni za Serikali pamoja na wananchi.
Kwa upande wa fedha zilizookolewa kutokana na kazi za uchunguzi na udhibiti, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Tanga katika kuzuia na kupambana na rushwa, wamefanikiwa kuokoa fedha taslimu shilingi milioi 117,714,374 zilizotokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya miamala ambayo haikuwa rafiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali.
"Pia ofisi imedhibiti kiasi cha Shilingi milioni 97,045,953, kiasi ambacho ni fedha za wananchi zilizofanyiwa ubadhilifu na hatimaye kiasi hicho kurejeshwa kwa wananchi. TAKUKURU Mkoa wa Tanga tumejiwekea mikakati ya kupunguza na kumaliza kero kwa wananchi hasa katika maeneo yanayoongoza kwa kulalamikiwa kuwa na vitendo vya rushwa. Mikakati hiyo ni pamoja na,
"Kuendelea kutoa elimu kwa umma katika makundi mbalimbali kuhusu athari mbalimbali za rushwa katika uchumi wa taifa letu na njia za kupambana na vitendo vya rushwa hususani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge.
"Kuendelea na udhibiti kwa kuchambua mifumo mbalimbali ili kubaini mianya ya rushwa na kushauri jinsi ya kuziba mianya hiyo kwa lengo au nia ya kudhiti rushwa kwenye mifumo husika.
"Kuendelea na kazi ya kufanya uchunguzi wa malalamiko ya vitendo vya rushwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya rushwa ili kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kutegemeana na ushahidi unaopatikana.Kuendelea kuwahamasisha wananchi kutoa ushirikiano hasa inapohitajika wao kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani,"amesema.
Pia amesema hatua nyingine ni kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali, hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, fedha za uboreshaji wa elimu bure, kufuatilia na kuhakiki kodi zinazopaswa kulipwa serikalini, maabara na maeneo mengine yahusuyo utekelezaji wa sera mbalimbali kwa lengo la kuokoa fedha za umma ili zitumike katika mambo yenye tija kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga.
"Kushirikisha wadau katika mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni sambamba na kutoa taarifa mbalimbali kwa umma ili kukidhi matakwa ya sheria mbalimbali na pia kufikia uhalisia wa shabaha ya TAKUKURU ya kufanya kazi pamoja na wadau wote katika mapambano dhidi ya rushwa na kuifanya kuwa jambo hatarishi na lisilo na manufaa kwa njia ya kuelimisha, kuzuia, kubaini na kuwafikisha watuhumiwa wote mahakamani.
"Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, tunawaomba na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla, kushiriki kwa namna mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa hususani kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.
Nichukue pia fursa hii kuwasihi wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa ili kwa pamoja tuweze kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kwamba viongozi waadilifu ndio wanapewa dhamana ya kuongoza kwa ridhaa ya wapiga kura.
"Kwa kufanya hivyo tutafikia lengo la kupunguza vitendo vya rushwa katika jamii na hatimaye kuvitokomeza kabisa kwani Tanzania bila rushwa inawezekana iwapo tutachagua viongozi wasiotoa rushwa. Natoa pia wito na ninawakaribisheni wananchi wote wenye taarifa za vitendo vya rushwa kwenye ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Tanga.
"Kwa wananchi waishio katika Jiji la Tanga wanaweza kutembelea ofisi yetu iliyopo eneo la Bombo karibu na Harbours Club, na kwa wale waishio wilayani wasisite kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo katika kila makao makuu ya wilaya zote za Mkoa wa Tanga.
"Aidha mwananchi au mdau yeyote anaweza kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga kwa namba zifuatazo:- 0689-797-998 na 0738-150-225(Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga), 0784-280-663 na 0738-150-228 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kilindi),0782-208-008 na 0738-150-232 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Muheza), 0784-290-117 na 0738-150-230 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Lushoto),0786-207-311 na 0738-150-233 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Pangani).
"Pia kwa namna 0782-866-867 na 0738-150-231(Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mkinga), 0713-442-425 na 0738-150-229 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Korogwe), 0688-313-853 na 0738-150-227 (Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Handeni). Pia wanaweza kupiga simu ya bure 113 au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kupiga *113# na kufuata maelekezo na kisha kutuoa ujumbe wako,"amefafanua kwa kina Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,Dkt. Sharifa O.Bungala.
Tags
Habari